Jan 24, 2024 06:57 UTC
  • Ghaza imeendelea kuwa makaburi ya halaiki ya wanajeshi vamizi wa Israel + VIDEO

Izzat al-Rishq, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, ukanda wa Ghaza utaendelea kuwa makaburi ya halaiki ya wanajeshi wa Israel waliouvamia ukanda huo na kwamba mfano wa wazi ni kuangamizwa wanajeshi 24 wa utawala wa Kizayuni kwa mkupuo mmoja siku chache zilizopita.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu kiongozi huyo mwandamizi wa HAMAS akisema hayo na kuongeza kuwa, tangu mwanzoni kabisa vya uvamizi wa Ghaza tuliwaonya Wazayuni kwamba eneo hilo litakuwa ni makaburi ya umati ya wanajeshi wa Israel. 

Vile vile amesema, utawala wa Kizayuni umeshindwa kufanikisha lengo angalau moja ililolitangaza wakati wa kuanzisha vita hivyo na kuongeza kuwa, matokeo ya vita vya hivi sasa yalijulikana tangu siku yake ya kwanza kabisa.

Matamshi hayo ya Izzat al-Rishq, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS yamekuja baada ya utawala wa Kizayuni kuchezea kipigo kikali kutoka kwa wanamuqawama wa Palestina. Wanajeshi 24 wa Israel wameangamizwa na idadi kubwa nyingine wamejeruhiwa hivi karibuni na wanamapambano wa Palestina. 

 

Jana usiku, Brigedi za Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS zilisambaza mkanda wa video wa operesheni yao ya siku ya Jumatatu iliyoangamiza na kujeruhi makumi ya wanajeshi vamizi wa Israel.

HAMAS imesema kuwa ilifanya operesheni hiyo juzi Jumatatu ndani ya majengo mawili walikokuwa wamejificha maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la utawala wa Kizayuni, mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya al Maghazi. Imesema ilitumia risasi mbili za RPG moja kupiga na kuteketeza kifaru na nyingine iliyopiga jengo lililokuwa limetegwa mabomu na kusababisha majengo mawili kuporomoka na kuangamiza wanajeshi wa Israel waliokuwa wamejificha huko.