Feb 15, 2024 07:49 UTC
  • Hashem Safieddine
    Hashem Safieddine

Afisa wa ngazi ya juu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amelaani mashambulizi ya hivi karibuni zaidi ya Israel kusini mwa Lebanon yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa wakiwemo watoto wawili, ikiapa kwamba majibu ya harakati ya Muqawama ya Lebanon yako njiani.

"Mashambulizi yaliyofanyika huko kusini mwa Lebanon, ambayo yameua idadi kadhaa ya raia, hayawezi kupita bila majibu. Hakika kutakuwa na jibu na litakuwa la kiwango kinachohitajika,” amesema Hashem Safieddine, mkuu wa Halmashauri Kuu ya Hizbullah.

Matamshi hayo yalikuwa jibu la kwanza la harakati ya Hizbullah kwa wimbi la mashambulizi ya Israel katika maeneo mbalimbali kusini mwa Lebanon.

Shirika la Habari la Taifa la Lebanon (NNA) limesema kuwa, ndege za kivita za Israel zililenga nyumba moja huko Sawwaneh katika shambulio "lililosababisha uharibifu" na kuua watu watatu wa familia moja.

NNA pia imesema shambulio la Israel lililolenga Adshit kusini mwa Lebanon limemuua mtu mmoja, ambaye Hizbullah imetangaza kuwa ni mmoja wa wapiganaji wake. Shambulio hilo pia liliwajeruhi watu wengine 10, kuharibu kabisa jengo na kusababisha uharibifu mkubwa kwa biashara, maduka na nyumba zilizo karibu.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel zimekuwa zikishambuliana karibu kila siku tangu utawala huo haramu ulipoanza mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya watu wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana.

Hizbullah inasema operesheni zake zinalenga kuunga mkono na kuwatetea wapigania ukombozi wa Ukanda wa Gaza.

Tags