Feb 20, 2024 07:06 UTC
  • UN: Jeshi la Israel limewabaka, limewapiga vibaya na kuwanyima chakula na dawa wanawake Wapalestina

Mamia ya wanawake na wasichana wa Kipalestina katika maeneo ya Ghazza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu wamekuwa wakiwekwa kizuizini kiholela na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel tangu Oktoba 7, na kuripoti kuwa wamebakwa, kupigwa vibaya na kunyimwa chakula na dawa na askari wa jeshi hilo.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameibua wasiwasi kuhusu "tuhuma za kuaminika za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu" unaofanywa na jeshi la Israel, ikiwa ni pamoja na aina nyingi za unyanyasaji wa kingono na ubakaji dhidi ya wanawake na wasichana wa Kipalestina huko Ghazza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Wataalamu hao wakiwemo maripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Reem Alsalem na Francesca Albanese ni sehemu ya chombo kikubwa zaidi cha wataalamu huru katika mfumo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa.

Wataalamu hao wameeleza katika ripoti yao: "wanawake na wasichana wa Kipalestina walioko kizuizini wamekabiliwa na aina nyingi za unyanyasaji wa kingono, ikiwemo kuvuliwa nguo na kupekuliwa na maafisa wa kiume wa jeshi la Israel".

Raeem Alsalem

Ripoti ya wataalamu hao wa UN imeendelea kueleza: "takribani wafungwa wawili wa kike wa Kipalestina waliripotiwa kubakwa huku wengine wakiripotiwa kutishiwa kubakwa na kunyanyaswa kingono".

Waliozuiliwa ni pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, ambao wanaripoti kufanyiwa "matendo ya kinyama na ya kudhalilisha."

Wanawake hao Wapalestina waliowekwa kizuizini wameorodhesha aina nyingi za unyanyasaji kama kupigwa vibaya, kunyimwa chakula, dawa na pedi za hedhi, na kupigwa picha katika "mazingira ya udhalilishaji" kisha kusambazwa mtandaoni na jeshi la Israel.

Ripoti moja ya kushangaza imetaja mwanamke wa Kipalestina aliyewekwa kizuizini huko Gaza na kuachwa nje kwenye kizimba bila ya chakula na katika mvua na baridi.

Wataalamu hao saba wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na madhubuti katika ripoti hizo, na kuitahadharisha Tel Aviv kuwa inapaswa kutoa ushirikiano kwa uchunguzi huo utakaofanywa.

Kwa mujibu wa habari walizopokea wataalamu hao wa UN, wanawake na wasichana wa Kipalestina wamelengwa na kuuawa makusudi huko Gaza, mara nyingi wakiwa pamoja na wanafamilia na watoto wao "mahali ambapo walitafuta hifadhi au wakati wakikimbia".

Kadhalika, imeelezwa katika ripoti ya wataalamu hao kwamba, baadhi ya wanawake hao Wapalestina waliripotiwa kushikilia vipande vyeupe vya vitambaa walipouawa na jeshi katili la utawala wa Kizayuni.

Aidha kuna idadi ya wanawake na watoto kadhaa wa Kipalestina huko Gaza ambao hawajulikani walipo tangu walipokumbana na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel.../

Tags