Feb 27, 2024 12:43 UTC
  • Aaron Bushnell
    Aaron Bushnell

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema serikali ya Marekani inabeba dhima ya kifo cha mwanajeshi wa nchi hiyo aliyejichoma moto nje ya Ubalozi wa Israel huko Washington akipinga uungaji mkono wa serikali ya Rais Joe Biden kwa mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel huko Ukanda wa Gaza.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema: "Utawala wa Biden unabeba dhima kamili ya kifo cha rubani wa Jeshi la Marekani, Aaron Bushnell, kutokana na sera zake zinazounga mkono mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni ya kuwaangamiza watu wa Palestina."

Hamas imeeleza kuwa: "Bushnell "ametoa mhanga maisha yake kwa shabaha ya kumulika mauaji ya kimbari na ya kizazi yanayofanywa na Wazayuni dhidi ya watu wetu katika Ukanda wa Gaza."

Hamas pia imetuma salamu za rambirambi na mshikamano wake kwa familia na marafiki wa rubani wa huyo wa Marekani, Aaron Bushnell.

Taarifa ya Hamas imesisitiza kuwa, rubani Aaron Bushnell amebakisha hai jina lake kama mtetezi wa maadili ya kibinadamu na mpinzani wa ukandamizaji dhidi ya watu wa Palestina ambao wanaendelea kuteseka kwa sababu ya utawala wa Marekani na sera zake za kidhalimu; kama ilivyokuwa kwa mwanaharakati wa Marekani, Rachel Corrie, ambaye alisagwasagwa na tingatinga la Israel huko Rafah mnamo 2003 (akiwatetea Wapalestina).

Hamas imeongeza kuwa, Rafah ni mji uleule ambao Bushnell amesabilia maisha yake ili kuishinikiza serikali ya nchi yake "izuie jeshi la wahalifu la Israel kuushambulia na kufanya mauaji na ukiukaji wa sheria huko."

Harakati ya Hamas imeendelea kwa kusema: "Rubani shujaa Aaron Bushnell atabaki milele katika kumbukumbu ya watu wetu wa Palestina na watu huru duniani, na ni ishara ya roho ya mshikamano wa kibinadamu wa kimataifa na watu wetu na mapambano yao ya kupigania haki."

Jana, Jumatatu, Aaron Bushnell alielekea katika ubalozi wa Israel mjini Washington. ambako alijimwagia petroli kichwani na nguoni na kujichoma moto huku akikariri kwa sauti kubwa: “Palestina Huru, Palestina Huru” hadi alipokata pumzi. Rubani huyo shujaa mtetezi wa Wapalestina aliaga dunia baadaye.