Mashambulio pacha ya jeshi la Kizayuni yaua Wapalestina 29 waliokuwa wakingojea msaada wa chakula Ghaza
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limewaua shahidi Wapalestina wapatao 29 wakati wakisubiri msaada katika mashambulizi mawili tofauti lililofanywa dhidi ya Ukanda wa Ghaza uliozingirwa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina huko Ghaza, katika tukio la kwanza la hapo jana Alkhamisi, Wapalestina wanane waliuawa shahidi katika shambulio la anga kwenye kituo cha usambazaji misaada katika kambi ya Al Nuseirat katikati mwa Ghaza.
Na katika kile kinachoonekana kama desturi yake hivi sasa, jeshi la Israel limekanusha kushambulia vituo vya misaada.
Mashambulizi ya kigaidi ya jeshi la Israel yamewafanya akthari ya Wapalestina zaidi ya milioni 2.3 walazimike kuyahama makazi yao.
Mnamo Februari 29, wanajeshi wa Israel waliwaua kwa risasi zaidi ya Wapalestina 100 walipokuwa wakisubiri kupatiwa msaada karibu na Mji wa Ghaza. Na kama kawaida yake, utawala wa Kizayuni ulijivua na dhima ya mauaji hayo na kuwalaumu Wapalestina waliouawa kwamba walijisababishia wenyewe vifo vyao.../