Mar 24, 2024 11:25 UTC
  • Hamas yalaani kimya cha dunia kuhusu uvamizi wa Israel kwenye hospitali ya al-Shifa ya Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (muqawama) ya Palestina, Hamas, imelaani vikali jamii ya kimataifa kwa "ukimya wake wa aibu" juu ya uvamizi wa jeshi la utawala wa Israel dhidi ya hospitali ya al-Shifa ya Gaza ambako maelfu ya Wapalestina waliokimbia makwao wanapata hifadhi.

Hamas imesema katika taarifa yake kwamba hujuma inayoendelea ya Israel dhidi ya hospitali hiyo inaashiria kufeli Umoja wa Mataifa na dunia nzima kwa ujumla katika kumshinikiza mshirika wa jadi wa Israel, Marekani, kuacha kupeleka silaha kwa utawala huo katili.

Ripoti hiyo  imeongeza kuwa jamii ya kimataifa imeshindwa kuzuia mauaji ya kimbari yanaotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina.  

Jeshi la Israel linaendelea kufanya mashambulizi ya anga na mizinga ndani na karibu na hospitali ya al-Shifa kwa siku ya saba mfululizo. Vyombo vya habari vinasema kuwa Wapalestina waliokimbilia hifadhi karibu na Hospitali ya al-Shifa hawana chakula na maji huku mashambulizi ya Israel yakiendelea.

Shirika rasmi la habari la Palestina Wafa, likinukuu vyanzo vya matibabu, limeripoti kwamba vikosi vya Israeli vinawazuilia wagonjwa wapatao 240 pamoja na wahudumu wa afya takribani 10 ndani ya hospitali hiyo, chini ya hali mbaya bila maji, chakula wala huduma za afya.

Watoto wa Gaza wakipata matibabu baada ya kudondoshewa mabomu na jeshi katili la Israel

Al-Shifa ilikuwa hospitali kubwa zaidi ya Ukanda wa Gaza kabla ya Israel kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo takribani miezi sita iliyopita.

Israel ilivamia kwa mara ya kwanza al-Shifa Novemba mwaka jana, ikisema kuwa Hamas ilitumia hospitali hiyo kama kituo cha kijeshi, madai ambayo Hamas imekanusha mara kadhaa. Utawala wa Israel haujatoa ushahidi wowote wa maana kuhusu madai yake hayo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, vituo vya afya 155 katika Ukanda wa Gaza vimeharibiwa tangu vita kuanza Oktoba mwaka jana.

Tangu kuanza kwa hujuma hiyo, utawala katili wa Israel umewaua Wapalestina wasiopungua 32,142 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kujeruhi watu wengine 74,412.