Apr 13, 2024 02:15 UTC
  • UNICEF: Watoto wa Ghaza wako taabani kwa kula nyasi

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF amesema, ameshuhudia kwa macho yake mtoto aliye taabani baada ya kula nyasi kutokana na njaa inayokabili mamia ya maelfu ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Tess Ingram, ameeleza hayo akiwa katika hospitali ya Al-Aqsa huko Deir al Balah katikati mwa Ukanda wa Ghaza na kuvionyesha vyombo vya habari mtoto wa Kipalestina aitwaye Omar, ambaye alifikishwa hospitalini hapo siku tatu zilizopita akitokea eneo la kaskazini mwa Ghaza na anapatiwa tiba dhidi ya utapiamlo.

Kwa mujibu wa Bi Ingram, bibi yake Omar alimfikisha mtoto huyo kwenye Hospitali ya Al-Aqsa baada ya kutengana na wazazi wake, na amepitisha muda wa wiki mbili akiwa anakula nyasi tu.

Ameongeza kuwa, mtoto huyo yuko kwenye machungu makubwa na ni miongoni mwa mamia ya watoto wanaotibiwa utapiamlo katika hospitali hiyo.

Msemaji huyo wa UNICEF ameongeza kuwa, watoto hao wana njaa na hawajapata chakula na tiba ya lishe ambayo wanahitaji na akatamatisha akisema “tunahitaji sitisho la mapigano hivi sasa.”

Tess Ingram

Wakati huohuo Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto limeeleza katika ujumbe lilioweka kwenye mtandao wa X kwamba, limeshawasilisha malalamiko  yake kwa mamlaka husika za utawala wa Kizayuni wa Israel na kubainisha kwamba, inasikitisha kuona watoa misaada wangali wanaendelea kukumbwa na hatari wakati wakisambaza misaada ya kibinadamu.

Katika ujumbe wake huo UNICEF imesema, misaada ya kibinadamu itafikia wahitaji pale tu watoa misaada hiyo watakapolindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA imesema, mabomu yanavyozidi kurindima, wakazi wa Ghaza wanahaha kuishi,  halikadhalika watoa misaada wanahaha kusambaza misaada ya kuokoa maisha.../

 

Tags