Apr 12, 2024 11:17 UTC
  • HAMAS: Kusitishwa vita kikamilifu ndio msingi wa kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni

Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, usitishaji vita wa kudumu ndio msingi mkuu wa kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel juu ya kuwarejesha makwao bila ya masharti yoyote Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao na kuondoka kikamilifu vikosi vya utawala huo katika Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Abdul Latif al-Qanou amesema: "kurejea bila masharti yoyote Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao na kuondoka kikamilifu vikosi vya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza ndicho kipaumbele chetu katika mchakato wa mazungumzo"; na akasisitiza kwamba: bila kutimizwa masharti hayo, hakuna mwafaka wowote utakaofikiwa.
 
Al-Qanou ameendelea kueleza kwamba, baada ya kupita miezi sita, Ghaza ingali iko imara na wala haitashindwa, na akaongezea kwa kusema: "ukubwa wa uharibifu na uangamizaji uliofanywa katika Ukanda wa Ghaza ni kielelezo kinachoakisi sura ya Unazi na Ufashisti ya utawala wa Kizayuni."
Abdul Latif al-Qanou

Msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa, Israel haitafikia malengo yake na akafafanua kwa kusema: kuendeleza vita kwa ajili ya kufanya mauaji ya halaiki, kusababisha baa la njaa na kurefusha muda wa vita hakutaufanya utawala wa Kizayuni uonekane mshindi au kuweza kufikia malengo yake.

Al-Qanou amesema, ukubwa wa jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni katika Hospitali ya Al-Shifa huko Ghaza ni wa kinyama na wa maafa makubwa na akaongeza kuwa, operesheni ya kutafuta waathirika, ya kufukua maiti za Mashahidi iliyoanza tangu siku 10 zilizopita ingali inaendelea.

Tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023 mbele ya kimya cha jamii ya kimataifa, hadi sasa haujasita kufanya jinai na unyama wa aina yoyote dhidi ya wananchi wa Palestina hasa wakazi wa eneo hilo.

Baada ya miezi sita, utawala wa Kizayuni haujapata mafanikio yoyote zaidi ya kufanya jinai, mauaji ya halaiki, uharibifu, jinai za kivita, ukiukaji wa sheria za kimataifa, kushambulia mashirika ya utoaji misaada na kuliweka kwenye hali ya njaa na mateso eneo la Ghaza.

Tangu vilipoanza vita dhidi ya eneo hilo lililowekewa mzingiro, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi hadi sasa imepindukia 33,634, mbali na wengine 76,214 waliojeruhiwa.../

 

Tags