Apr 18, 2024 11:00 UTC
  • UN:  Israel inaendeleza vikwazo haramu vya misaada kwa watu wa Gaza

Msemaji na Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa utawala haramu wa Israel unaendeleza vikwazo visivyo halali vya katika uwanja wa kupeleka misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza.

Shirika la Habari la IRNA limeripoti kuwa, Ravina Shamdasani, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva kuwa Israel inaendelea kuweka vikwazo visivyo halali vya kuingia na kusambaza misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na inaendelea kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Shamdasani ameongeza kuwa, mchakato wa kupeleka misaada ya kibinadamu huko Gaza umevurugika, na licha ya madai ya utawala wa Kizayuni na Washington kuhusu mtiririko wa misaada hiyo katika siku za hivi karibuni, mashirika yenye uhusiano na Umoja wa Mataifa yanasema kiwango cha misaada hiyo kimefikia kiwango cha chini kabisa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kimsingi.

Gaza

Msemaji huyo wa Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa, licha ya ukosoaji mkubwa dhidi ya hatua za Wazayuni, lakini Israel inadai kuwa misaada ya kibinadamu inaendelea kupelekwa Gaza.

Shamdsani amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukikabiliwa na mashinikizo yanayoongezeka duniani ya kuruhusu shehena za misaada kuingia Gaza baada ya shambulio lake la Aprili 1 lililoua wafanyakazi wa kimataifa wa kutoa misaada ya kibinadamu huko ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, idadi ya mashahidi waliouawa na jeshi la utawala wa Kizayuni huko Gaza imefikia watu elfu 33, na 843 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia watu elfu 76, 575.

Asilimia 73 ya wahanga wa mashambulizi hayo ni wanawake na watoto.

Tags