Apr 21, 2024 07:52 UTC
  • Haniyeh: Marekani inailinda kisiasa Israel mkabala wa mauaji ya kimbari ya utawala huo

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameikosoa Marekani kwa kuzuia kutambuliwa taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa, akiishutumu Washington kuwa inaipatia Israel ulinzi wa kisiasa kwa mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.

Ismail Haniyeh Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kuwa makumi ya maelfu ya watu katika Ukanda wa Gaza wameuliwa shahidi kwa kutumia silaha za Marekani na kwamba hatua ya Washington ya kulipigia kura ya veto ombi kwa ajili ya kuasisi nchi ya Palestina katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni wazi kuwa inatoa ulinzi wa kisiasa kwa jinai ya ukatili wa Israel dhidi ya wakazi wa Gaza. 

Haniyeh ameongeza kuwa maelfu ya watu wameuawa shahidi kwa silaha, makombora na uuungaji mkono wa Marekani kwa hujuma katili za utawala wa Kizayuni. Kitendo cha Marekani cha kulipiga veto ombi hilo kuhusu Palestina kinamaanisha kuwa Marekani inatoa ulinzi kamili na ruhusa kwa Israel kuendeleza mauaji ya kimbari na ukatili dhidi ya Gaza. 

Mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza 

Akizungumza katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ametahadharisha juu ya oparesheni tarajiwa ya kijeshi ya jeshi la Israel dhidi ya Rafah na kusema itasababisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. 

Haniyeh amesisitiza kuwa utawala wa Israel haujakubali kusitisha vita  Ukanda Gaza licha ya mazungumzo yote kwani mapendekezo kadhaa yamewasilishwa kupitia wapatanishi.

 

Tags