Apr 26, 2024 03:06 UTC
  • UN: Hatuwezi kuwaambia Wapalestina wasubiri misaada

Jumuiya ya kimataifa ina jukumu na wajibu wa kufanya kazi kufanikisha kukwamua Gaza lakini hatuwezi kuwaambia raia Wapalestina wanaoteseka wasubiri, amesema afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na ufikishaji wa misaada kwenye eneo hilo linalokabiliwa na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala haramu wa Israel.

Sigrid Kaag, ambaye ni Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi mpya wa Gaza, amesema machungu makubwa yanayosababishwa na miezi ya mashambulizi ya makombora nayo pia lazima  yapatiwe ufumbuzi.

Bi. Kaag ameyasema hayo Alhamisi akiwa  jijini New York, kuhutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Bi. Kaag ametangaza mfumo mpya wa kuingiza Gaza misaada ya kuokoa maisha, mfumo ambao utaanza siku chache zijazo.

Ni takribani miezi saba sasa tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kwa lengo la kukabiliana na Wapigania ukombozi wa Palestina.

Wizara ya Afya Gaza inasema zaidi ya Wapalestina 34,000 wameuawa shahidi Gaza na zaidi ya 77,000 wamejeruhiwa, wengi wakiwa ni wanawke na watoto tangu Israel ianzishe vita dhidi ya Gaza Okotoba saba mwaka jana.

Kaaga amesema ametembelea Gaza hivi karibuni ili kupata taarifa kadri iwezekanavyo kuhusu changamoto zilizoko. Amesema kile nilichoona maeneo mbalimbali ya Gaza ni kiwango kikubwa cha uharibifu na kuongeza kuwa Wapalestina wanaishi katika mazingira haya yasiyo ya kiutu kabisa kutokana na vita vya utawala katili wa Israel dhidi ya eneo hilo.