Matokeo ya hatua ya kijinai ya utawala wa Kizayuni ya kuishambulia Rafah
Kitendo cha jinai cha utawala wa Kizayuni cha kushambulia makazi na mahema ya wakimbizi wa Kipalestina katika mji wa Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza kitakuwa na taathira mbalimbali kwa viongozi watenda jinai wa utawala huo haramu katika ngazi ya kieneo na kimataifa.
Juzi usiku jeshi la Kizayuni lilishambulia kwa mabomu kambi zaidi ya kumi na mahema ya wakimbizi wa Kipalestina katika mji wa Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza na matokeo yake Wapalestina wasiopungua 190 wakiwemo wanawake na watoto waliuawa shahidi na wengine makumi kujeruhiwa.
Harakati za muqawama wa Kiislamu wa Palestina (Hamas); na Jihadul Islami siku ya Jumatatu tarehe 27 Mei, 2024 katika taarifa tofauti zilitoa radiamali kuhusiana na mauaji ya jeshi la utawala wa Kizayuni kaskazini-magharibi mwa mji wa Rafah na kuitaja jinai hiyo kuwa ni kupuuza waziwazi na kuidharau hukumu ya hivi karibuni ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) juu ya haja ya kukomeshwa mashambulizi katika mji huo na Rais wa Marekani Joe Biden na serikali ya nchi hiyo wanawajibika kwa uhalifu huo unaoendelea huko mji wa Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza.
Harakati za muqawama wa Kiislamu wa Palestina za Hamas Jihadul Islami zilitangaza kuwa hazitashiriki katika mazungumzo yoyote baada ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika kambi ya wakimbizi ya mji wa Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza.
Wanajeshi wa jeshi la Misri pia walirusha risasi kuelekea vikosi vya utawala wa Kizayuni kwenye kivuko cha Rafah. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri iliutaka utawala wa Kizayuni ukiwa ni utawala vamizi utekeleze hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ya kusimamisha mara moja operesheni za kijeshi na hatua nyinginezo huko Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza.
Moja ya mipango ya utawala wa Kizayuni baada ya kushindwa na makundi ya muqawama ya Palestina huko ukanda wa Gaza imekuwa ni kutumia mbinu zisizo za kibinadamu na za kinyama.

Katika miezi ya hivi karibuni wanajeshi wa Kizayuni wameshambulia mara kwa mara maeneo ya mikusanyiko ya Wapalestina huko ukanda wa Gaza na vitendo hivyo vya jinai vinazingatiwa kuwa ni mauaji ya kimbari kwa mujibu wa taasisi na mashirika ya kimataifa.
Wakuu wa utawala huo ghasibu wa Kizayuni kwa kulenga kambi za Wapalestina waliopoteza makazi yao kutokana ikiwa ni natija ya sera za vita za Wazayuni, wanataka kutekeleza mpango wao mchafu na usio wa kibinadamu kwa ajili ya kuwahamisha kwa lazima wakazi wa ukanda wa Gaza.
Tel Aviv pia inafanya njama za kuongeza ukosefu wa usalama katika eneo hilo na kwa kuzingatia mpaka wa Rafah na Misri isogeze mapigano kwenye maeneo ya mpaka wa nchi hiyo.
Matukio ya miezi michache iliyopita huko Gaza yamedhihirisha wazi kwamba njama na malengo maovu ya viongozi watenda jinai wa utawala wa Kizayuni ya kukabiliana na makundi ya muqawama wa Palestina hazitafanikiwa na kwamba makundi hayo yatakabiliana na Wazayuni kwa umoja na mshikamano mkubwa zaidi. Harakati za muqawama wa Kiislamu wa Palestina kwa kutumia mikakati mbalimbali na madhubuti yameweza kuwashinda wavamizi hao katika nyanja tofauti na kuchukua hatua ya kuendeleza malengo yao na kuwa wahusika wakuu katika medani ya vita.

Baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala huo wanakaribia kusambaratika kutokana na kushindwa mfululizo katika vita vya ukanda wa Gaza na kwa namna fulani mashambulizi ya kikatili ya jeshi la Kizayuni dhidi ya wanawake na watoto ni kitendo cha kukata tamaa na kutokuwa na uwezo katika vita vya ukanda wa Gaza.
Jinai za Wazayuni huko mji wa Rafah kusini mwa ukanda wa Gaza zitakuwa na matokeo ya mabaya kieneo na kimataifa.
Katika upande wa kieneo, makundi ya muqawama yatapanua wigo wa mashambulizi yao dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa mshikamano mkubwa zaidi. Katika uga wa kimataifa rekodi mbaya dhidi ya haki za binadamu ya utawala wa Kizayuni itaandaa uwanja kupandishwa kizimbani viongozi watenda jinai wa utawala huo ghasibu.