Dec 29, 2020 02:59 UTC
  • Nukta muhimu katika mahojiano ya Sayyid Hassan Nasrallah na Televisheni ya Al Mayadeen

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah Jumapili 27 Disemba alifanya mahojiano muhimu na Televisheni ya Al Mayadeen ya Lebanon. Katika mahojiano hayo aliwakumbuka na kuwawenzi Shahidi Luteni Jenerali Hajj Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis.

Aidha alibainisha nukta kadhaa ambazo ni muhimu katika kufahamu hali ya sasa katika eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati hasa sera za maadui wa kambi ya muqawama au mapambano ya Kiislamu.

Nukta ya kwanza ni kuhusu namna Marekani, Israel na Saudi Arabia zinavyotumia mauaji kufikia malengo yao

Moja ya nukta muhimu katika hotuba ya Jumapili usiku ya Sayyid Hassan Nasrallah ni kuhusu namna pande tatu za Marekani, Israel na Saudi Arabia ambazo ni mahasimu wakuu wa harakati ya muqawama, zilivyoshirikiana kuwaua Luteni Jenerali Shahidi Qassem Soleimani na Shahidi Abu Mahdi al Muhandis. Amesema baada ya Marekani, Israel na Saudia kupata pigo katika makabiliano na harakati za muqawama, ziliamua kudhoofisha harakati hiyo kwa kuwaua kigaidi  Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis. Sayyid Nasrallah amefichua kuwa Saudia, Marekani na Israel zinapanga njama ya kumuua yeye bianfsi pia.

Sayyid Hassarn Nasrallah amebainisha maudhui mbili zaidi kuhusu mhimili huo wa pande tatu wa shari unaojumuisha Saudia, Marekani na Israel. Maudhui ya kwanza aliyoashiria ni kuwa mbinu ya mauaji imebadilika. Sayyid Hassan Nasrallah amesema mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis  yalikuwa ni ya wazi wazi kinyume na mauaji ya Emad Mughniyeh. Mbali na kuwa ya wazi mauaji hayo yalitekelezwa kwa ushirikiano wa Saudia, Marekani na Israel. Mauaji ya Emad Mughniyeh hayakuwa ya wazi na Israel iliyatekeleza peke yake lakini hivi sasa wapinzani wa muqawama wanashirikiana na wanatekeleza mauaji yao wazi wazi. Nutka hii inaonyesha kuwa, hivi sasa mauaji ya kigaidi ni sera maalumu ambayo inatekelezwa na wapinzani wa harakati za mapambano ya Kiislamu au muqawama kama njia ya kukabiliana na harakati hizo.

 Mashahidi Abu Mahdi al Muhandis na Qassem Soleimani 

 

Maudhui nyingine hapo ni kuwa , adui ana ufahamu potovu kuwa harakati za muqawama zitasambaratishwa kwa kuuawa kigaidi makamanda wao. Sayyid Hassan Nasrallah aliashiria nukta hiyo na kusisitiza kuwa, mhimili wa muqawama hautegemei watu kadhaa ambao wakiuawa unakuwa ndio mwisho wa mhimili huo. Amebaini kuwa harakati za muqawama hazifiki ukiongoni kwa kuuawa makamanda wake wa ngazi za juu bali hupata nguvu zaidi.  Hii ni nukta ambayo wapinzani wa harakati za mapambano ya Kiislamu au muqawama hawajaweza kuidiriki vyema.

Nukta ya pili ni kuhusu uanzishwaji uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kufichuka ukweli kuhusu fikra za baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu.

Moja ya nukta muhimu katika mahojiano ya Sayyid Hassan Nasrallah Jumapili usiku ni kuhusu hatua ya baadhi ya tawala za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel. Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco ni nchi ambazo katika mwaka wa 2020 zimeanzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni. Watawala wa nchi hizo za Kiarabu katika miaka ya nyuma pia walikuwa na uhusiano wa siri na Israel lakini walikuwa wakitoa nara za kuwaunga mkono Wapalestina ili kuhadaa mataifa yao lakini sasa taswira halisi ya tawala hizo imedhihirika. Kuhusiana na maudhi hii Sayyid Hassan Nasrallah amesema:  “Uhaini wa watawala wa nchi za Kiarabu kwa Palestina ni zaidi ya inavyobainika hadharaini. Usaliti huu ndio sasa umedhihirika kadamnasi. Kwa hakika kadhia ya Palestina ilikuwa mzigo kwa watawala wa nchi hizo za Kiarabu. Kwa hivyo hatua yao ya kuanzisha uhusiano na Israel imeweka wazi unafiki na udumakuwili wao.

Nukta ya tatu ni kuwa, Hizbullah na harakati zingine zote za muqawama zimepata nguvu na zimeimarika zaidi ya wakati wowote mwingine ule.

Shahidi Emad Mughniyeh

 

Maudhui nyingine muhimu katika mahojiano ya Al Mayadeen na ‘Sayyid wa Muqawama’ ilikuwa sisitizo kuhusu uwezo wa Hizbullah na harakati za muqawama katika kuwazuia maadui. Hapa aliashiria nukta mbili.

Kwanza ni kuwa, Hizbullah italipiza kisasi baada ya Israel kumuua shahidi Ali Kamel Mohsen . Sisitizo hilo la Sayyid Hassan Nasrallah ni ishara kuwa, Hizbullah huzingatia ‘zama’ katika hatua inazochukua. Kuchelewa katika kulipiza kisasi kuuawa shahidi wapiganaji wa Hizbullah huwa ni kwa sababu ya mazingira ya kisiasa na kiusalama Lebanon lakini hilo haliathiri msingi muhimu wa ulipizaji kisasi.

Maudhui nyingine aliyoashiria Sayyid Hassan Nasrallah ni kuwa, makombora ya Hizbullah yameongezeka mara mbili zaidi ya mwaka uliopita na makombora hayo yanaweza kulenga kwa ustadi mkubwa eneo lolote ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel. Maudhui hii inaonyesha kuwa Hizbullah sasa ina uwezo mkubwa wa kumzuia adui na hiyo ni kengele ya hatari kwa adui kuwa, uamuzi wowote wa kijeshi atakaouchukua atakabiliwa na uwezo mkubwa wa harakati ya muqawama ya Lebanon.

 

Tags