Jul 24, 2022 02:23 UTC
  • Ansarullah yalaani vikali mwandishi wa habari mzayuni kukanyaga ardhi tukufu ya Makka

Ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen imelaani vikali hatua ya Saudi Arabia ya kutoa kibali kwa mwandishi wa habari mzayuni wa Israel kufika kwenye ardhi tukufu ya Makka.

Gil Tamari, mwandishi wa habari Myahudi wa chaneli ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel, alifika hadi mji mtukufu wa Makka wakati wa ziara ya hivi karibuni aliyofanya rais Joe Biden wa Marekani nchini Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Masirah, ofisi ya kisiasa ya Ansarullah ya Yemen imetoa taarifa ikisisitiza kuwa safari ya mwandishi wa habari wa chaneli ya kizayuni mjini Makka, kwenye mlima wa Arafa na maeneo mengine matakatifu, imeyakanyaga na kuyavunjia heshima waziwazi matukufu ya Kiislamu na kuzichochea hisia za Waislamu duniani.

Al Kaaba na Msikiti mtukufu wa Makka

Katika taarifa yake hiyo, harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu nchini Yemen imebainisha kuwa, utoaji suhula ambao utawala wa Saudia umezingatia kwa ajili ya Wayahudi, unafanywa katika hali ambayo, utawala huo umewazuia mamilioni ya Waislamu kuelekea Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada tukufu ya Hija.

Kupitia taarifa yake hiyo, Ansarullah imewataka Waislamu duniani wachukue msimamo madhubuti na hatua athirifu na ya pamoja dhidi ya sera za Saudi Arabia, ambazo kwa mujibu wa viongozi wa harakati hiyo ya muqawama ya Yemen, zimelenga kuhujumu umma wa Waislamu, mapiganio yao matukufu na matakatifu yao.

Siku chache baada ya kumalizika ziara ya rais wa Marekani Joe Biden nchini Saudi Arabia, Gil Tamari amesambaza video katika mtandao wa kijamii wa Twitter inayomuonyesha akiwa katika maeneo mbalimbali ya ardhi tukufu ya Makka likiwemo eneo la Arafa.

Video hiyo imeamsha hasira za Waislamu hata ndani ya Saudia yenyewe pia wakisisitiza kuwa huko ni kuuvunjia heshima mji mtakatifu wa Makka ambao ni marufuku kuingia kwa wasio Waislamu.../

 

 

 

Tags