Dec 01, 2022 04:01 UTC
  • Bunge la Kuwait lapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel

Wabunge wa Kuwait wamepinga vikali hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Wabunge hao sambamba na kutangaza upinzani wao kwa hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel wamesisitiza himaya na uungaji mkono wao kwa taifa la Palestina

Taarifa ya Wabunge hao imetolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Wapalestina iliyoadhimishwa Novemba 29 na kusisitiza juu ya udharura wa kuongezwa himaya na uungaji mkono kwa muqawama na mapambano ya Palestina.

Wabunge wa Kuwait wamesisitiza katika taarifa yao pia kwamba, kuna haja kwa viongozi wa utawala ghasibu wa Israel kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutokana na kutenda jinai za kivita huko Palestina.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Wabunge wa Kuwait imesisitiza kwamba, Wapalestina wana haki ya kuendesha mapambano dhidi ya maghasibu wa Wazayuni mpaka haki zao zilizoghusubiwa zitakaporejeshwa na kwamba, hilo ni katika matakwa ta kimsingi ya serikali na wananchi wa Kuwait

Maandamano ya kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel

 

Wabunge wa Kuwait wameyataka pia mataifa ya Kiarabu na Kiislamu sambamba na kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina wafuatilie mchakato wa kushtakiwa viongozi wa Israel katika Mahakama ya Kimataiifa ya Jinai (ICC).

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Marzouq Ali Mohammed Al-Ghanim, Spika wa Bunge la Kuwait amenukuliwa mara kadhaa akisisitiza kuwa, msimamo wa nchi yake kuhusiana na Palestina uko thabiti na si wenye kubadilika na kwamba, nchi hiyo inapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.   

Tags