Indhari ya Wapalestina kuhusiana na kuendelea njama dhidi ya Masjidul-Aqswa
Kushtadi njama za Wazayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa katika siku za hivi karibuni ambazo zimesadifiana na kumbukumbu ya kuchomwa moto msikiti huo na Wazayuni maghasibu kumepelekea kuibuka wasiwasi mkubwa miongoni mwa Wapalestina na fikra za waliowengi ulimwenguni.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Palestina Jumatatu ya jana tarehe 21 Agosti ilitoa taarifa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuchomwa moto msikiti wa al-Aqswa na Wazayuni mwaka 1969 na kutangaza kuwa, njama dhidi ya kibla hiki cha kwanza cha Waislamu zingali zinaendelea na kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel ungali unafuatilia hatua zake za kutaka kuudhibiti kikamilifu msikiti huo.
Moja ya hatua na njama kubwa za kuuharibu na kuubomoa msikiti wa al-Aqswa ni ile iliyotekelezwa Agosti 21 mwaka 1969 yaani miaka 48 iliyopita, ambapo Wazayuni wenye kufurutu ada wakiongozwa na Denis Michael Rohan walitekeleza mpango ulioratibiwa na viongozi wa Israel na kuuchoma moto msikiti wa al-Aqswa. Kitendo hicho kilipelekea sehemu ya msikiti huo mtakatifu kuharibiwa vibaya.
Kwa hakika hakuna wakati ambao maeneo ya mji wa Baitul-Muqaddas na Masjdul-Aqswa yalisalimika na njama za Wazayuni wenye kufurutu ada.
Daima viongozi wa utawala vamizi wa Israel wamekuwa wakiandaa mipango ya kuyaharibu na kuyabomoa maeneo ya kihistoria ya Baitul Muqaddas. Tangu mwaka 1967, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya njama za kila namna za kutaka kufuta athari za mji huo mkongwe na wa kihistoria wa Baitul-Muqaddas.
Hujuma na mashambulio ya kuratibiwa ya Wazayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa kwa shabaha ya kuuchoma moto msikiti huo, kuubomoa kupitia uchimbaji mashimo na njia za chini kwa chini za kuelekea katika msikiti huo, kuuzingira, kuwazuia waumini kuingia katika msikiti huo kwa ajili ya kutekeleza ibada na kuwavamia waumini hao kwa ajili ya kuzusha hofu na wahaka ni miongoni mwa njama za kila namna za Wazayuni huko Baitul-Muqaddas ambazo zingali zinaendelea kushuhudiwa hadi leo hii.
Katika mwendelezo wa njama hizo, kila siku walowezi wa Kizayuni wakipata himaya na ulinzi wa polisi na maafisa wa Shirika la Kijasusi la Israel MOSSAD wamekuwa wakiuvamia msikiti huo na kutaka kuugawa kiwakati na kimahali. Wazayuni wanataka kuugawa msikiti huo kiwakati na kimahali ili sambamba na kuwaruhusu Wazayuni kuingia katika eneo hilo takatifu wapate fursa mwafaka pia ya kusukuma mbele gurudumu la siasa zao za kupenda kujitanua.
Hatua hizo za Israel kwa hakika zina lengo la kupima fikra za waliowengi ulimwenguni kuhusiana na siasa zake hizo za kufanya uharibifu dhidi ya msikiti wa al-Aqswa.
Njama za uharibifu za utawala haramu wa Israel zinaendelea kushuhudiwa katika hali ambayo, mji wa Baitul-Muqaddas ni chimbuko la dini za mbinguni na mahala walipopita Manabii wa Allah na eneo ambalo kwa miaka nenda rudi limekuwa likiheshimiwa na kutukuzwa na dini za Uislamu, Uyahudi na Ukristo.
Katika kipindi cha miongo kadhaa ya kukaliwa kwa mabavu Baitul-Muqaddas, mji huo mkongwe mara kadhaa umekabiliwa na hujuma na mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika mazingira kama haya, bila shaka kuna udharura zaidi kwa jamii ya kimataifa kuwa macho mkabala na njama za utawala wa Kizayuni wa Israel; na hili ndilo jambo linalosisitizwa na kutiliwa mkazo daima na wananchi madhulumu wa Palestina.