Aug 04, 2018 01:25 UTC
  • Uingiliaji wa Marekani katika zoezi la kuarifisha Waziri Mkuu mpya wa Iraq

Marekani imeyataarifa makundi mbalimbali ya Iraq kwamba Haider al-Abadi ndiye chaguo la Washington kwa ajili ya nafasi ya Waziri Mkuu mpya wa Iraq.

Uchaguzi wa nne wa Bunge la Iraq ulifanyika tarehe 12 Mei mwaka huu. Kazi muhimu zaidi baada ya uchaguzi huo ni kuainisha Waziri Mkuu wa serikali ya Baghdad. Hata hivyo imepita miezi mitatu sasa baada ya uchaguzi huo bila ya makundi mbalimbali ya kisiasa kuafikiana juu ya nani atachukua nafasi ya Waziri Mkuu wa serikali ijayo ya Baghdad. 

Kunatajwa mambo kadhaa yanayoweza kuwa sababu ya kuahirishwa suala la kuteuliwa Waziri Mkuu mpya wa Iraq. Hassan Shukripour ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kistratijia anaamini kuwa: Sababu kubwa ya suala hilo ni kukaribiana sana idadi ya viti vya Bunge vya makundi tofauti ya kisiasa na tofauti kubwa iliyopo baina ya idadi ya viti vya kundi la Sairuuna lililopata viti vingi zaidi yaani viti 54 vya Bunge, na kura zinavyohitajika (165) kwa ajili ya kuweza kuarifisha Waziri Mkuu. Hii ni kwa sababu hitilafu hiyo kubwa inatatiza kazi ya kupatikana muungano wa vyama na makundi kadhaa kwa ajili ya kupata wingi mutlaki wa kura 165 na kuweza kuarifisha Waziri Mkuu.

Bunge la Iraq

Mbali na hayo, uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Iraq una umuhimu mkubwa sana katika mchakato wa kuainisha Waziri Mkuu wa serikali ijayo. Marekani ni miongoni mwa serikali zinazoingilia sana masuala ya ndani ya Iraq. Gazeti la al Sharq al Ausat limeandika kuwa: Marekani imeyaarifu makundi mbalimbali ya Iraq kwamba Waziri Mkuu wa sasa wa nchi hiyo Haider al-Abadi ndiye chaguo pekee la serikali ya Washington kwa ajili ya nafasi ya Waziri Mkuu. Gazeti hilo limeandika kuwa: Baadhi ya jumbe za Marekani kwa makundi ya kisiasa ya Iraq zilikuwa na lugha kali na hata vitisho na tahadhari kwamba, iwapo miungano mbalimbali itamchagua mtu mwingine asiyeungwa mkono na Washington yatawekewa vikwazo na Marekani. 

Sisitizo la Marekani la kuteuliwa al Abadi kuwa Waziri Mkuu wa serikali mpya ya Iraq limetolewa licha ya kundi lake la al Nasr kupata viti 42 na kushika nafasi ya pili baada ya lile la Sairuun linaloongozwa na Muqtada Sadr ambalo limepata viti 54 vya Bunge. Kundi la tatu la al Fat'h linaloongozwa na al Amiri limepata viti 47 vya Bunge.

Muqtada Sadr

Katika upande mwingine ili kuweza kumuarifisha al Abadi kuwa Waziri Mkuu kunahitajika mwafaka wa makundi mengine na kupata wingi mutlaki wa kura 165 za Bunge. Hata hivyo na kwa kutilia maanani mgawanyo wa viti vya Bunge jipya, al Abadi hawezi kupata nafasi ya kuwa Waziri Mkuu bila ya kupata ridhaa ya vyama na makundi ya Kishia kwa ajili ya kuunda muungano imara na wenye nguvu.

Suala jingine ni kuwa, Marekani inakwamisha mchakato wa kuchaguliwa Waziri Mkuu mpya wa Iraq huku ikijulikana wazi kwamba, miongoni mwa nara muhimu za makundi ya Sairuuna na al Fat'h yaliyopata vingi vingi zaidi vya Bunge ilikuwa kupinga uingiliaji wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya Iraq.

Inaonekana kuwa, uingiliaji wa Marekani katika mchakato wa kurifisha Waziri Mkuu mpya wa Iraq una malengo mawili. Kwanza ni kuwa Marekani inataka kuzuaia uundwaji wa muungano baina ya makundi ya Kishia bila ya kushirikisha lile la al Nasr, na pili ni kuwa, iwapo al Abadi ataarifishwa kuwa Waziri Mkuu wa serikali mpya basi ipate kujigamba kwamba, uteuzi huo umetokana na tahadhari zake na kwa njia hiyo kuonesha kwamba ina nafasi na ushawishi mkubwa nchini Iraq.          

Tags