Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-3
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya tatu ya kipindi hiki kipya cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Katika kipindi kilichopita tuliashiria misingi ya ubeberu kwa mtazamo wa Imamu Khomeini ambapo tulisema kuwa, kupitia muhimili wa dini ya Uislamu na mafundisho ya Ushia, kupambana na ubeberu na watumiaji mabavu wa ndani na nje, ndio msingi wa mapambano ya kisiasa ya mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Na ni kwa aji hiyo katika muundo na ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, kupambana na mfumo wa kibeberu na kupigania kujitawala kisiasa, kukawa moja ya matukufu na nara za wananchi. Kadhalika tulisema kuwa, katika kipindi cha kupigwa nara za kupambana na uistikbari, Imamu Khomeini alitoa pendekezo kwamba, dunia iliyo chini ya anga ya mihimili miwili ya kipindi cha vita baridi na katika maeneo mengi ya dunia, watu wangepiga nara dhidi ya ubepari ambao kimsingi ulikuwa na sifa na alama ya Umaksi. Hata hivyo Imamu Khomeini na kwa ushujaa aliweka wazi kwa kuzitangaza kambi zote mbili yaani Marekani na Urusi ya Zamani kuwa ni dhihirisho la ubeberu wa dunia sambamba na kuzishambulia kwa kutumia nara ya 'Si Mashariki Si Magharibi' kupitia ramani ya siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hiki tunakusudia kukuleteeni aina nyingine ya fikra za kisiasa ya Imamu Khomeini, ambayo ni uadilifu wa kijamii.
*********
Ndugu wasikilizaji, kufikiwa uadilifu wa kijamii ni moja ya daghadagha za kibinaadamu katika kipindi chote cha historia na malengo makuu ya wananchi wa Iran katika mapinduzi ya o ya Kiislamu. Katika hali ambayo katika miaka ya baadaye na baada ya Vita vya Pili vya Dunia, kambi ya Mashariki kwa usimamizi wa Muungano wa Urusi ya Zamani na kwa kutegemea maelekezo ya Umaksi na Ujamaa, ilidai uungaji mkono wa uadilifu wa kijamii na kuondoa ubaguzi ndani ya jamii. Kwa kutumia fikra hiyo, dini ilionekana kuwa inaunga mkono dhulma katika tabaka la watu wanyonge na madhaifu wa jamii hiyo. Hata hivyo Imamu Khomeini na kwa kutegemea mafundisho ya dini ya Uislamu na madhehebu ya Ushia, alipiga nara ya uadilifu wa kijamii ili kwa njia hiyo iwezekane kufikiwa matukufu ya taifa la Iran. Itakumbukwa kwamba, mapambano mapana kwa ajili ya kufikiwa uadilifu wa kijamii, yalianza tangu karne ya 19 Miladia, hata hivyo na licha ya kufikiwa kwa baadhi ya mafanikio na kukaribia ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, bado ilikuwa vigumu kuweka mfumo ambao ungaweza kutetea watu wa tabaka masikini katika jamii na kulingania mwito wa kuondoa dhulma na ubaguzi katika jamii ya Iran. Imamu Khomeini (MA) na kwa uongozi wake wa busara, alibadili linganio la uadilifu wa kijamii kuwa moja ya nara muhimu na takwa la wananchi katika harakati za mapinduzi ya Kiislamu, na akalipa kipaumbele suala la kufikiwa uadilifu wa kijamii na kuondoa ubaguzi kupitia msingi wa kuainishwa siasa za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
********
Kwa kuzingatia nafasi ya Uislamu na madhehebu ya Ushia katika mtazamo wa fikra wa Imamu Khomeini, ilikuwa suala la dharura kubainisha mitazamo yake kuhusiana na kadhia ya uadilifu wa kijamii, nafasi ya kwanza na umuhimu wa uadilifu katika maktaba ya Uislamu. Hata hivyo ndugu wasikilizaji mnafahamu kwamba uadilifu ni moja ya maana za misingi ya nadharia ya kisiasa na hadi sasa wataalamu wa falsafa na wasomi wengi wamejitahidi kulifafanua suala hilo. Kila mtu miongoni mwa wana nadharia hao, alijitahidi kubainisha upana wa malengo mazito ya suala la uadilifu wa kijamii. Katika kipindi cha mfumo wa Magharibi, wanafalsafa wakubwa kama vile Plato na Aristotle wa Ugiriki na kadhalika katika kipindi cha Uislamu, wanafikra kama vile Al-Farabi na pia wananadhia wengi wa kileo, nao walijitahidi kubainisha maana ya uadilifu katika mitazamo yao binafsi. Katika dini ya Uislamu na madhehebu ya Shia pia, uadilifu umepewa nafasi kubwa kama ambavyo ni moja ya misingi ya madhehebu ya Shia. Aidha kusifiwa Mwenyezi Mungu na sifa ya uadilifu, limeakisiwa kwa umuhimu katika fikra ya Ushia, kupitia mitazamo ya kisiasa na kijamii ya wanafikra na maulama wa madhehebu hayo.
********
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu tatu ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia kiini na kichochezi cha Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya usimamizi wa Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Qur’an Tukufu imeutaja uadilifu kuwa msingi ambao uwezo umejengeka juu yake na uongozi bora wa ulimwengu unafikiwa kupitia jambo hilo. Katika mwenendo huo, ndipo uadilifu ukawa ni msingi na chanzo cha uwezo na dira kuu ya ulimwengu na wanadamu, ambapo lengo la mwisho la wanadamu, ni kufikiwa uadilifu huo na kuueneza katika jamii. Aidha kwa mtazamo wa Qur’an, uadilifu una utukufu wa dhati, ambapo usalama na amani vyote vinategemea jambo hilo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akawataka wanadamu wote hususan waumini kufanya uadilifu na usawa. Kwa mtazamo wa Qur’an, uadilifu una chimbuko katika fitra ya mwanadamu na ili kufikiwa uadilifu na usawa katika pande zote za maisha ya mwanadamu na katika masuala yote ya kijamii, wanadamu wanatakiwa kufanya juhudi endelevu kwa ajili ya kuudumisha. Katika uwanja huo, Qur’an Tukufu inawataja wale wanaofanya juhudi kwa ajili ya kufikiwa uadilifu katika jamii kuwa ni ‘wapenzi wa Mwenyezi Mungu’ kwa kusema: “….Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu.” Surat Maidah aya ya 42. Ni kwa msingi wa fikra hiyo na itikadi ambayo ilifundishwa na Mtume Muhammad (saw) na watu wake wa karibu, ndipo Imamu Khomeini (MA) akalivalia njuga suala la uadilifu wa kijamii.
*********
Kiini cha mtazamo na matendo ya Imamu Khomeini katika kufuatilia lengo la kufikiwa uadilifu wa kijamii katika jamii, ni Mtume Muhammad (saw) na Imamu Ali Bin Abi Twalib (as). Hii ni kwa kuwa katika maisha yote ya Mtume huyo wa Allah (saw) daima alikuwa akilingania na kupigania sula la kuimarisha uadilifu na kuondoa dhuluma dhidi ya watu wanyonge na masikini. Mtume wa Allah katika kipindi cha utume wake alifanya juhudi kubainisha malengo ya uadilifu wa kijamii kwa mtazamo wa dini ya Uislamu. Lengo kuu likiwa ni kusafisha mtazamo wa watu na kuandaa mazingira ya kupatikana jamii ya uadilifu. Kwa mtazamo wa fikra ya dini ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, uadilifu wa kijamii ni wenye pande tofauti na upande wa kwanza ni usawa katika uumbwaji wa wanadamu. Kwa mujibu wa Nabii huyo wa Allah, wanadamu wote kwa tofauti zao za rangi, lugha, kaumu na kabila, wako sawa na wanadamu wengine na hakuna mtu mwenye ubora juu ya mwngine ispokuwa tu kwa uchaji-Mungu. Aidha kwa mujibu wa Mtume wa Uislamu, wanadamu wote wako sawa katika uumbaji na natija yake ni kwamba, kuanzia uhuru na hiari wako sawa kwa ajili ya kuainisha mustakbali wao. Mtume huyo alisisitiza kwamba wanadamu wote wako sawa kama ambavyo pia ni ndugu na ili kufikia jamii ya uadilifu ni lazima wote kwa pamoja waweze kushirikiana. Sambamba na kuwahimiza Waislamu juu ya udugu, aliwataka kuunda jamii iliyojengeka juu ya uadilifu na usawa mbali na dhulma na ubaguzi. Katika dini ya Mtume wa Uislamu, maana ya uadilifu, usawa, insafu na kulinda haki za wengine, kimsingi ni mambo ambayo yanaunda jamii moja iliyo salama na inayotakiwa.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya tatu ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.