Serikali ya Iraq yasambaratisha genge la kigaidi mjini Baghdad
(last modified Mon, 18 Sep 2023 10:45:27 GMT )
Sep 18, 2023 10:45 UTC
  • Serikali ya Iraq yasambaratisha genge la kigaidi mjini Baghdad

Shirika la Usalama wa Taifa la Iraq limetangaza habari ya kusambaratishwa na kutiwa mbaroni kanali ya kigaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.

Mwaka 2017 na baada ya kupita miaka mitatu ya kutekwa maeneo mengi ya Iraq na genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS), serikali ya Iraq ilitangaza kuangamizwa genge hilo.

Pamoja na hayo, baadhi ya wanachama wa Daesh wamebakia na wamejificha ndani ya jamii hasa katika mikoa kama ya Diyala, Kirkuk, Nainawa, Salahuddin, al Anbar na Baghdad. Mara kwa mara magaidi hao wanafanya mashambulizi ya hapa na pale ya kigaidi na ya kuvizia kwenye mikoa hiyo.

Maafisa wa Iraq katika operesheni ya kusafisha mabaki na hasara zilizosambabishwa na magaidi wa Daesh

 

Kwa mujibu wa televisheni ya Al Mayadeen, Shirika la Usalama wa Taifa la Iraq limetangaza kuwa, wanachama wa genge hilo walituma magaidi wao kufanya operesheni za kujiripua kwa mabomu dhidi ya misafara ya maashiki wa Imam Husain waliokuwa wanaelekea kwenye maeneo ya kufanyia ziara nchini humo.

Polisi wa Iraq wamesema kuwa, magaidi hao walikuwa wamekusudia pia kufanya mashambulizi katika vituo vya polisi, masoko na maeneo ya makazi ya watu mjini Baghdad lakini vikosi vya usalama vya Iraq vimefanikiwa kulisambaratisha genge hilo.

Taarifa ya Shirika la Usalama wa Taifa la Iraq amesema kuwa, wanachama wa genge hilo la kigaidi wamekiri kuwa, walikuwa wamepewa mafunzo makubwa ya kutengeneza mabomu na mikanda ya kujiripua.

Vikosi vya usalama vya Iraq vimesema kwamba, vinaendelea na operesheni zao za kuyasafisha mabaki ya magaidi wa Daesh katika kona zote za nchi hiyo ya Kiarabu.