Umuhimu wa safari ya Bashar al Assad huko China
(last modified Sat, 23 Sep 2023 11:32:36 GMT )
Sep 23, 2023 11:32 UTC
  • Umuhimu wa safari ya Bashar al Assad huko China

Rais Bashar al Assad wa Syria Alhamisi ya juzi tarehe 21 Septemba aliwasili katika mji wa Hangzhou mashariki wa China kwa lengo la kushiriki katika hafla ya ufunguzi wa michezo ya Asia ya Hangzhou na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Xi Jin Ping wa nchi hiyo.

Uchambuzi wa safari ya Bashar al Assad nchini China unapaswa kufanywa kwa kzingatia maslahi ya Damascus na Beijing. Syria iliathiriwa na vita vya ndani tangu mwaka 2011; vita ambavyo sasa vimepungua  kwa kiasi kikubwa ijapokuwa baadhi ya maeneo ya nchi hiyo bado yanashikiliwa na makundi ya kigaidi na mengine yanakaliwa kwa mabavu na nchi majeshi ya nchi ajinabi. Katika miaka miwili ya karibuni, siasa za baadhi ya nchi zinazowaunga mkono wapinzani na makundi ya kigaidi huko Syria zimebadilika na zimeanza kuhuisha uhusiano wao na Damascus. Aghalabu ya nchi za Kiarabu, ikiwemo Saudi Arabia na Imarati, tayari zimehuisha uhusiano wao na Syria na zimetangaza kuwa ziko tayari kuijenga upya nchi hiyo. Aidha Syria nayo imerejea katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League). Ziara ya Bashar al Assad huko Beijing nchini China inaweza kutajwa kuwa ni katika muendelezo wa mchakato huu; suala linaloashiria namna Syria inavyojiondoa katika kipindi cha kutengwa.  

Suala jingine ni kuwa, Bashar al Assad mara ya mwisho alifanya safari mjini Beijing mwaka 2004 ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Hu Jin Tao, kiongozi wa zamani wa China. Ziara ya mwaka 2004 ya Bashar al Assad huko China ilikuwa safari ya kwanza kufanywa na Rais wa serikali ya nchi hiyo huko China tangu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo mwaka 1956. Kwa msingi huo, ziara ya sasa ya Assad mjini Beijing ni ya pili kuwahi kufanywa na Rais wa serikali ya Damascus huko China na pia ni mazungumzo ya kwanza kufanyika kati ya Bashar al Assad na Xi Jinping huko Beijing. 

Rais Bashar al Assad wa Syria ziarani mjini Beijing,China 

Jambo la tatu pia ni kuwa, Syria baada ya muongo mmoja wa vita ambavyo vimesababisha uharibifu mkubwa na kubomolewa karibu asilimia 80 ya miundombinu ya nchi hiyo, inahitaji uwekezaji wa kigeni kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo. China hii leo inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa duniani ambayo ina uwezo na suhula zinazohitajika kwa ajili ya kuwekeza katika nchi mbalimbali duniani. Kwa msingi huo, Assad anataraji kuwa China itakuwa na nafasi na mchango muhimu katika kuijenga upya Syria.  

Hii ni kusema kuwa, ziara ya Assad nchini China ina umuhimu kwa serikali ya nchi hiyo. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, China imezidisha juhudi za kidiplomasia katika eneo la Asia Magharibi, khususan jitihada zake za kusaidia kuondoa hali ya mvutano kati ya Iran na Saudi Arabia mwezi Machi mwaka huu. Inaonekana kuwa, China inafanya kila iwezalo kuzidisha uhusiano wake na Syria khususan katika sekta ya uchumi. Duru za habari za Syria zimeripoti kuwa, Rais wa China ametoa ndege yake mahsusi kwa ajili ya safari ya Rais Bashar al Assad wa Syria na ujumbe aliofuatana nao huko China; kitendo kinachoonyesha kiwango cha umuhimu wa safari hiyo kwa serikali ya Beijing. 

Mao Ning, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema: "Tunaamini kuwa ziara hii ya Rais Bashar al Assad wa Syria itapanua hali ya kuaminiana kisiasa na ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali kati ya nchi mbili, na wakati huo huo kukuza uhusiano wa pande mbili katika ngazi mpya. China na Syria zina urafiki mkubwa wa jadi unaorejea miaka 76 nyuma; na uhusiano wa nchi mbili hizi umekuwa ukipanuka na kustawi."  

Mao Ning, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China 

Na nukta ya mwisho ni kuwa, ziara ya Assad mjini Beijing imefanyika wakati huu ambapo Beijing inajiandaa kuwa mwenyeji wa "Mkutano wa Ukanda na Barabara" ambao utaanza mwezi ujao ukihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 100 duniani. China inatilia maanani na kutoa kipaumbele kwa suala la ukamilishaji wa mradi wake wa kukuza uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo na kusaidia kuendeleza miundombinu yake yenyewe.