Ansarullah yatangaza kushikamana na taifa la Syria
(last modified Fri, 06 Oct 2023 07:10:47 GMT )
Oct 06, 2023 07:10 UTC
  • Ansarullah yatangaza kushikamana na taifa la Syria

Ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen imelaani mashambulizi ya makundi ya kigaidi katika chuo cha kijeshi cha Homs nchini Syria.

Televisheni rasmi ya Syria ilitangaza jana Oktoba 5 kuhusu shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye sherehe za kuhitimu wahitimu wa chuo cha kijeshi katika mkoa wa Homs.

Hasan al-Ghabash, Waziri wa Afya wa Syria, alitangaza kuwa kwa mujibu wa takwimu za awali, idadi ya mashahidi wa jinai hiyo ya kigaidi ni watu 80, wakiwemo watoto sita na wanawake sita, na idadi ya waliojeruhiwa imefikia takriban watu 240. Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, ofisi ya kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen sambamba na kulaani hujuma ya makundi ya kigaidi dhidi ya chuo cha kijeshi katika mji wa Homs, imesisitiza kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni zinajinufaisha na jinai hiyo.

Ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Ansarullah imetangaza katika taarifa yake kwamba kitendo hicho cha jinai kimefichua ukatili wa makundi ya kitakfiri yanayoungwa mkono na Marekani na utawala wa Kizayuni.

Taarifa hiyo imesema: "Marekani na utawala wa Kizayuni ndizo zinazonufaika na jinai hiyo iliyodhidi ya taifa, uongozi na jeshi la Syria.

Katika taarifa hiyo harakati ya Ansarullah imesisitiza kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni ziko nyuma ya njama zote za kikatili dhidi ya taifa la Syria, na kwamba jambo hilo linatokana na  misimamo ya Syria ya kuunga mkono Palestina, siasa zake za mhimili  wa muqawama na upinzani dhidi ya kuboreshwa uhusiano na utawala huo ghasibu. Ansarullah pia imetangaza mshikamano wake kamili na taifa la Syria katika kupambana na ugaidi na njama za Marekani na utawala wa Kizayuni.