Operesheni ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Ghaza
Katika muendelezo wa mashambulizi ya kikatili ya vikosi vya utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza, misikiti na hospitali za eneo hilo bado ni shabaha ya makusudi ya mashambulizi hayo.
Katika kuendeleza mashambulizi yake ya jinai dhidi ya maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza, makombora ya utawala wa Kizayuni yamelenga na kuharibu minara ya misikiti iliyo karibu na barabara ya al-Dawa iliyoko katika kambi ya Nusirat katika ukanda huo. Utawala wa Kizayuni si tu haujatosheka na kushadidisha mateso ya wagonjwa wa saratani katika Ukanda wa Ghaza kwa kuwanyima dawa ua kutotoa kibali cha kusafiri kwao nje ya ukanda huo kwa ajili ya kupata matibabu yanayofaa, bali unataka kuwaua kwa umati wagonjwa hao kupitia mashambulizi makali ya mara kwa mara kandokando ya hospitali hiyo na kujaribu kuiharibu au kuishambulia moja kwa moja kwa mabomu.
Ili kuwahamisha kwa nguvu wahudumu wa afya na wakimbizi katika Hospitali ya Al-Aqsa, vikosi vya utawala ghasibu wa Israel vimeshambulia kwa mabomu eneo la karibu na hospitali hiyo mara 25 na kwa mujibu wa tangazo rasmi, zaidi ya Wapalestina 8100 wameuawa shahidi wengi wao, kwa mujibu wa UNICEF, wakiwa ni watoto na wanawake. Wavamizi hao ambao wamethibitisha unyama wao katika jinai za kulipua kwa makusudi Hospitali ya Al-Maamadani na mauaji ya wanawake na watoto, wameongeza vitisho vyao vya kuzishambulia hospitali nyingine, ikiwemo Hospitali ya Quds katika siku chache zilizopita.
Mashambulio makali ya mabomu katika hospitali ya al-Shafa, mojawapo ya vituo vikuu vya matibabu katika Ukanda wa Ghaza, yalianza baada ya mashambulio ya mabomu katika hospitali tatu za Al-Quds, Uturuki na al-Aqsa. Mashambulizi hayo yalifanyika baada ya utawala huo ghasibu kutoa mara kadhaa indhari ya kuhamishwa wagonjwa, lakini jambo hilo halikuwezekana kutokana na hali ya vita kutoruhusu majeruhi na wagonjwa wengine mahtuti kuhamishiwa katika hospitali salama.
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ameeleza wasiwasi wake kuhusu maonyo kama hayo yanayotolewa na utawala wa Kizayuni ya kutaka kuhamishwa wagonjwa katika hospitali ya Quds na kueleza kuwa, kamwe haiwezekani wagonjwa kuondolewa kwenye hospitali ambazo tayari zimejaa wagonjwa mahututi.
Huduma za afya zinapaswa kufanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Mashambulizi ya mabomu katika vituo vya matibabu huko Ghaza yanaendelea katika hali ambayo harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Hamas imeonya katika taarifa zake kuhusu uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya mabomu katika hospitali za Ghaza na hivyo kutokea maafa mengine katika ukanda huo.
Tokea kuanza mashambulizi hayo ya kikatili, utawala ghasibu wa Quds umewaua shahidi madaktari 116, waokoaji 18 na waandishi habari na wanaharakati wengine wa vyombo vya habari 35.
Mfuko wa Kimataifa wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesisitiza kuwa, hali ya watoto huko Ghaza ni ya kutisha sana na idadi ya waliouawa miongoni mwao ni ya maafa.
Katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera, msemaji wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kulindwa hospitali za Ghaza na kufunguliwa vivuko kwa ajili ya kutumwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza.
Hali ya wakazi wa Ghaza inaendelea kuwa mbaya sana kwa kukatwa huduma za kimsingi kama vile maji na umeme. Kuongezeka mashinikizo dhidi ya wakimbizi na waomba hifadhi wa Kipalestina kunatoa kipaumbele kwa suala la kupelekwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo. Hata hivyo utawala wa Kizayuni unawazuia wakazi wa eneo hilo kupata misaada ya kimataifa kwa kukwamisha na kuchelewesha mambo na hii ni pamoja na kuwa kiasi cha misaada iliyopokelewa huko hailingani na mahitaji ya Wapalestina wanaoishi katika ukanda huo.
Kipande kimoja cha mkate na glasi ya maji mdio mgao wa kila siku kwa kila mtoto wa Kipalestina katika misaada duni ya kimataifa inayofikishwa Ghaza kwa matatizo makubwa. Kwa kufungwa njia za kufikishwa mafuta Ghaza, utendaji wa mitambo ya kuzalisha umeme kwenye hospitali za ukanda huo umefikia kiwango cha chini kabisa na sasa kuna hatari kubwa ya kusimama kabisa shughuli za kila siku za hosptilahi hizo.
Hata kama utawala wa kibaguzi wa Israel unatoa visingizio vya kukabiliana na matokeo ya mashambulio ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa kama sababu ya kudumisha mashambulio yake ya kinyama dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza, lakini ushahidi uliopo unaonyesha kuwa hata kabla ya kutekelezwa operesheni hiyo, tayari serikali ya mrengo wa kulia ya Netanyahu ilikuwa na mipango ya kuwafukuza wakazi wa Ghaza kutoka ukanda huo.
Kuhusu suala hilo, gazeti la mrengo wa kushoto la Haaretz limefichua njama ya mpango hatari ambao ulikuwa umepangwa na shirika la kijasusi la utawala haramu wa Israel wa kuwahamishia wakazi wa Ukanda wa Ghaza katika jangwa la Sinai nchini Misri, siku moja moja baada ya kumalizika vita.
Kwa mujibu wa mpango huo, ili utawala wa Israel uweze kuutekeleza kwa mafanikio kwanza utalazimika kusimika mahema katika miji ya kaskazini mwa Sinai na kisha kujenga huko makazi ya kudumu kwa ajili ya watu waliohamishwa kutoka Ghaza.
Kwa kuzingatia mpango huo hatari, inafahamika wazi ni kwa nini utawala huo unalipua na kubomoa kwa makusudi mejengo ya makazi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Unadondosha kwa makusudi matani ya mabomu yenye uharibifu mkubwa kwenye majengo marefu na ya makazi huko Ghaza ambapo katika kipindi cha chini ya wiki tatu za mashambulio, umeweza kuwafanya zaidi ya wakazi milioni moja kati ya wakazi wote milioni mbili na laki tatu wa ukanda huo kuwa wakimbizi wanaohitaji misaada ya dharura ya kibinadamu, misaada ambayo imekuwa vigumu kuwafikia wahanga hao kutokana na mzingiro wa kikatili unaotekelezwa dhidi yao na Wazayuni wanaokalia kwa mabavu ardhi zao.