Sababu za umuhimu wa kuingia Yemen katika vita vya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i104552-sababu_za_umuhimu_wa_kuingia_yemen_katika_vita_vya_gaza
Katika hali ambayo nchi muhimu za Kiarabu hazijachukua hatua yoyote ya maana mkabala wa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na kujiri maafa ya binadamu katika ukanda huo, serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen yenye makao yake huko Sana'a imetangaza rasmi kuingia vitani dhidi ya utawala wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 09, 2023 07:11 UTC
  • Sababu za umuhimu wa kuingia Yemen katika vita vya Gaza

Katika hali ambayo nchi muhimu za Kiarabu hazijachukua hatua yoyote ya maana mkabala wa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na kujiri maafa ya binadamu katika ukanda huo, serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen yenye makao yake huko Sana'a imetangaza rasmi kuingia vitani dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Wayemeni walitekeleza shambulio lao la kwanza la anga dhidi ya Israel tarehe 20 mwezi Oktoba mwaka huu ambapo walirusha ndege zisizo na rubani na makombora kadhaa katika anga ya Bahari Nyekundu. Shambulio hilo lilisambaratrishwa na manowari ya jeshi la majini la Marekani. Brigedia Jenerali Yahya Saree Msemaji wa Jeshi la Yemen tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka huu alitangaza rasmi kuwa jeshi hilo limeyashambulia baadhi ya maeneo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Saree aliongeza kuwa shambulio la Oktoba 31 lilikuwa shambulio la tatu kufanywa na jeshi la Yemen. 

Msemaji wa jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree 

Sababu kuu iliyopelekea Wayemeni waingie vitani huko Gaza ni kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa eneo hilo. Uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni pia ni sababu nyingine ya kuchukuliwa hatua hiyo. Sayyid Abdulmalik al Houthi Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ametangaza baada ya uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni kuwa harakati hiyo inawasiliana na iko pamoja na mhimili wa muqawama na kwamba, iwapo Marekani itaingilia kijeshi moja kwa moja huko Gaza, basi watakuwa tayari pia kushiriki moja kwa moja katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaani droni. Yahya Saree amesisitiza kuwa, na hapa ninamnukuu; "Tunapaswa kutekeleza wajibu wetu kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na kulisaidia taifa linalodhulumiwa na azizi la Palestina dhidi ya mashambulizi ya kikatili ya Marekani na Israel huko Ukanda wa Gaza. 

Sayyid Abdulmaliki al Houthi 

Kuingia rasmi Yemen katika vita vya Ukanda wa Gaza kuna umuhimu mkubwa na wakati huo huo kunatoa ujumbe maalumu.  Ujumbe wa kwanza ni kuwa: Kuingia moja kwa moja  harakati ya Ansraullah katika vita dhidi ya Israel kunamaanisha kufunguliwa upande wa tatu wa vita baada ya Hizbullah ya Lebanon. Harakati hii ya tatu inaweza kubadili sehemu ya nguvu za ulinzi na oparesheni za Israel. Kwa msingi huo, kuingia Wayemeni vitani huko Gaza ni sawa na kudhihirisha umoja na mshikamano katika harakati ya muqawama. 

Ujumbe wa pili, ni tahadhari ya utawala wa Kizayuni na hata Marekani ya kuendeleza na kupanua vita huko Gaza. Hata kama hadi sasa harakati ya Hizbullah imetumia sehemu ndogo tu ya uwezo wake huku Wayemeni pia wakiwa wametekeleza mashambulizi machache, lakini iwapo utawala wa Kizayuni utaendeleza jinai zake huko Gaza; makundi ya muqawama yanaweza na yako tayari kutumia suhula na uwezo wao wote kukakbiliana na utawala huo ghasibu. 

Ujumbe wa tatu ni kwamba; Wayemen ambao katika kipindi cha miaka 9 ya karibuni wamekabiliana na uvamizi wa nchi ajinabi, na hawatishwi wala kuhofia vita vingine vyovyote dhidi yao; wana irada na azma thabiti inayohitajika kwa ajili ya kupambana na Wazayuni, kwa sababu tayari utawala wa Kizayuni umeikalia kwa mabavu sehemu ya kijiografia ya kusini mwa Yemen. Weledi wa mambo wanasema kuwa kutohofia vita ni suala muhimu katika kuchambua nyenendo na hatua za Wayemen. Katika uwanja huo, Fabian Hinz Mtafiti katika Taasisi ya Kimataifa ya Institute for Strategic Studies (IISS) anasema: Kwa pande za kikanda ambazo zinataka kuilenga Israel, Yemen ndipo mahali panapofaa zaidi kwa ajili ya shughuli hiyo. Kwa mtazamo wa kisiasa na kistratejia, Yemen ni sehemu maalumu kwa ajili ya mhimili wa muqawama kwa sababu hakuna hatari ya kufanyika vita vya maafa kama ilivyo Lebanon. Hinz pia ameashiria uwezekano wa Israel kutekeleza mashambulizi ya anga ya kulipiza kisasi au Marekani na kusema: Hatua kama hizi haziwezi kuwazuia Wayemen. Hii ni kwa sababu licha ya kuwa ni hatari na za kuogofya, lakini wamezizoea. "