Jul 03, 2016 07:22 UTC
  • 80 wauawa katika mashambulizi ya mabomu Baghdad, Iraq

Watu wasiopungua 80 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi pacha ya mabomu katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Hujuma ya kwanza imeripotiwa kufanyika alfajiri ya leo nje ya mgahawa mmoja katika wilaya ya Karada na muda mfupi baadaye shambulizi la pili likafuatia mashariki mwa Baghdad.

Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Baghdad awali ilisema watu zaidi ya 60 wameuawa na wengine 100 wamejeruhiwa. Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limekiri kuhusika na mashambulizi hayo na kutoa takwimu tofauti na za serikali za wahanga wa hujuma hizo. Matakfiri hao wamesema Waislamu 40 wa madhehebu ya Shia wameuawa katika mashambulizi hayo na wengine 80 wamejeruhiwa.

Mashambulizi hayo yamefanyika masaa machache baada ya Waziri Mkuu wa Iraq kuzionya pande zinazowaunga mkono wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Haider al-Abadi aliyasema hayo jana Jumamosi katika kikao na waandishi wa habari mjini Baghdad, na kuongeza kuwa, wale walioanzisha kundi la kigaidi la Daesh au kuliunga mkono, hivi sasa wanateketea katika moto ambao waliuwasha wao wenyewe.

Hujuma hii inafanyika siku mbili baada ya watu 46 kuuawa na kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi dhidi ya msikiti mmoja katika kitongoji cha Abu Ghraib, viungani mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Tags