Safari ya kihistoria ya Rais Pezeshkian nchini Iraq, yenye matokeo chanya na ya wazi
(last modified Sun, 15 Sep 2024 10:33:57 GMT )
Sep 15, 2024 10:33 UTC
  • Safari ya kihistoria ya Rais Pezeshkian nchini Iraq, yenye matokeo chanya na ya wazi

Safari ya siku tatu ya Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Iraq imemalizika katika hali ambayo matokeo ya safari hiyo yanaonekana kuwa chanya na ya wazi kabisa katika kuimarisha umoja na mshikamano wa mataifa mawili.

Nchi ya Iraq inachukuliwa kuwa nchi iliyo karibu zaidi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kijiografia na kisiasa. Iraq ina mpaka wenye urefu wa zaidi ya kilomita 1450 na Iran ambapo siasa zake katika miongo miwili iliyopita, zimekuwa ni za kuimarisha uhusiano na kuishi kwa amani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Dalili ya mwenendo huo mzuri unaozidi kukua na mtazamo chanya wa Wairaqi kuhusu uhusiano na Iran ni hatua ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Muhammad Shia al Sudan ya kwenda kumlaki mwenyewe Rais Masoud Pezeshkian na ujumbe wa ngazi ya juu wa Iran aliofuatana nao. Al-Sudani akiwa pamoja na mawaziri wake kadhaa walikwenda moja kwa moja kwenye uwanja wa ndege kumlaki rasmi Pezeshkian badala ya hafla hiyo kufanyika katika uwanja wa Ikulu ya Waziri Mkuu.

Rais Masoud Pezeshkian akiwa safarini mjini Baghdad

Nechirvan Barzani, rais wa utawala wa ndani wa eneo la Kurdistan la Iraq, pia binafsi alikwenda kumkaribisha rasmi Rais Masoud Pezeshkian na ujumbe wa ngazi ya juu wa Iran aliofuatana nao katika uwanja wa ndege wa Erbil na hata kuzungumza kwa lugha ya Kifarsi katika mahojiano na mwandishi wa habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wakati wa safari yake nchini Iraq, Rais Pezeshkian alifanya mambo vitofauti kabisa na marais wengine wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo mara hii safari yake haikuishia Baghdad na miji ya kidini pekee, bali mbali na Baghdad na miji ya Najaf na Karbala, Rais Pezeshkian na wenzake aliofatana nao pia walisafiri hadi Erbil na Basra. Kwa hakika Rais Pezeshkian huku akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa Iran alitembelea maeneo yote muhimu ya Iraq kutoka Baghdad, kitovu cha Iraq hadi Basra iliyoko kusini kabisa na Erbil na Sulaymaniyah katika majimbo ya kaskazini kabisa mwa Iraq na hatimaye Karbala na Najaf katika maeneo ya Furati ya Kati.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba safari ya Pezeshkian haikuishia tu kwenye mikutano ya kisiasa na rasmi na viongozi wa Iraq, bali pamoja na mikutano hiyo, alikutana na kuzungumza pia na wafanyabiashara wa Iran na wanaharakati wa masuala ya kiuchumi wanaofanya kazi nchini Iraq, familia za Wairani na matabaka tofauti ya watu wakiwemo viongozi wa makabila na wasomi wa Iraq. Wakati huo huo, safari ya Erbil, Sulaymaniyah na Basra ilifanyika katika safari ya kwanza kabisa ya Rais Pezeshkian nchini Iraqi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa rais wa Iran kutembelea maeneo ya Kurdistan na Basra.

Mbali na hayo, ikumbukwe pia kuwa viongozi wa Iran na Iraq walitia saini hati 14 za ushirikiano katika nyanja mbalimbali katika safari hiyo, na inaonekana kuwa wameazimia kuongeza kiwango cha biashara kati yao juu ya kiwango cha sasa cha dola bilioni 12. Vyombo vya habari vya Iraq vimetaja kutiwa saini kwa hati hizi za ushirikiano kuwa ni "ushirikiano wa kimkakati kati ya Iraq na Iran.

Rais Pezeshkian wa Iran na viongozi wa Iraq wamesisitiza nia ya serikali zao ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na wa kieneo

Nukta muhimu ya mwisho ni kwamba safari ya siku tatu ya Rais wa Iran nchini Iraq kwa mara nyingine tena imethibitisha kuwa Baghdad na Tehran zimeshikamana na kupaza sauti moja ya kupinga jinai na siasa za kikatili za utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa madhulumu la Palestina. Katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari, Muhammad Shia al-Sudani Waziri Mkuu wa Iraq na  Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kauli moja walilaani jinai hizo za kinyama zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa kuna ulazima wa kusitishwa mauaji ya kimbari dhidi ya watu hao haraka iwezekanavyo. Iwapo sauti moja hiyo itaenea katika nchi nyingine za Kiislamu bila shaka, kama alivyosisitiza Rais Pezeshkian akiwa nchini Iraq, utawala katili wa Kizayuni hautathubutu kuwaua Waislamu kwa umati, kama unavyofanya hivi sasa huko Ukanda wa Gaza.

Tags