Indhari kuhusu kukaririwa Nakba ya pili huko Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i104956-indhari_kuhusu_kukaririwa_nakba_ya_pili_huko_palestina
Maafisa wa Umoja wa Mataifa sambamba na kutahadharisha kuwa, utawala wa Kizayuni unapanga kukariri Nakba ya pili huko Gaza, wametangaza kuwa, Israel inatumia mbinu ya kukata mawasiliano ya simu na Intaneti kuficha jinai zake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2023 02:32 UTC
  • Indhari kuhusu kukaririwa Nakba ya pili huko Palestina

Maafisa wa Umoja wa Mataifa sambamba na kutahadharisha kuwa, utawala wa Kizayuni unapanga kukariri Nakba ya pili huko Gaza, wametangaza kuwa, Israel inatumia mbinu ya kukata mawasiliano ya simu na Intaneti kuficha jinai zake.

Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa ametoa indhari hiyo katika mahojiano na gazeti la Uingereza la Financial Times na kueleza kwamba, matokeo ya tathmini ya umoja huo yanaonyesha kuwa, Israel haitawaruhusu wakimbizi wa Gaza kurudi kaskazini mwa eneo hilo. Israel inasema kuwa inawatafuta viongozi wa Hamas kusini mwa Gaza, na hii inamaanisha kuwafukuza wakaazi wa eneo hilo kutoka huko.

Mamlaka za utawala ghasibu wa Israel zimetoa mara kwa mara mwito wa kuhamishwa kwa wingi kwa wakimbizi wa Gaza na kuhamishiwa katika jangwa la Sinai nchini Misri au kupelekwa katika nchi za Kiarabu na Ulaya.

Wakati huo huo, kumefichuliwa nyaraka kuhusu jicho la tamaa la utawala wa Kizayuni kwa hifadhi ya mafuta na gesi iliyogunduliwa katika pwani ya Gaza, jambo ambalo linafichua malengo ya nyuma ya pazia ya utawala huo wa Kizayuni ya kuanzisha vita dhidi ya Gaza na kuonesha kuwa utawala huo ghasibu una mipango ya kuikalia kwa mabavu na kuidhibiti Gaza. Inaonekana kuwa, hiyo ndio ajenda hasa ya Israel kabla hata ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqswa.

Kwa kuzingatia hili, inawezekana kusema kuwa, majanga yaleyale yaliyotokea baada ya kukaliwa kwa mabavu Palestina mwaka 1948 yanaweza kurudiwa sasa, na hii ina maana kwamba, wigo wa vita vya Gaza hautabakia katika mipaka ya Gaza pekee.

Mei 1948 Wazayuni walivamia, kuua na kuwafukuza Wapalestina 750,000 katika miji yao na kuharibu takriban vijiji 530

 

Tarehe 15 Mei 1948, ambayo inajulikana kwa jina la "Nakba" katika historia ya Palestina, ni siku ambayo Wazayuni walivamia, kuua na kuwafukuza Wapalestina 750,000 katika miji yao na kuharibu takriban vijiji 530. Walowezi wa Kizayuni hata walichukua hatua ya kubadilisha majina asilia ya vijiji na miji hiyo na kuipa majina mapya ya Kiyahudi ili kurahisisha juhudi za kupora na kuwapa makazi Mayahudi katika maeneo hayo.

Siku ya Nakba sio tu ni nembo ya maafa yaliyowapata Wapalestina tangu mwaka huo, bali pia inawakilisha masaibu na matatizo ambayo yametwishwa taifa la Palestina katika miongo kadhaa iliyopita. Kwa hakika, "Siku ya Nakba" ni kisa cha msiba na maafa ya kibinadamu yaliyopelekea kuharibiwa sehemu kubwa ya misingi ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kisheria ya Wapalestina ili kuandaa uwanja wa kutangazwa uwepo wa utawala haramu.

Baada ya majeshi ya Uingereza kuondoka kutoka Palestina, usiku wa manane Mei 14, 1948, kulitangazwa kuanzishwa kwa serikali ya Israel na mwenendo wa uvamizi huo ukashika kasi.

Katika kipindi chote cha siku za baada ya Nakba mnamo 1948, Wapalestina wasiopungua elfu 15 waliuawa shahidi na Wapalestina wengine elfu 750 walifukuzwa kutoka katika nchi yao. Idadi hii ilikuwa zaidi ya nusu ya wakazi wa Palestina wakati huo. Kiujumla, asilimia 70 ya Wapalestina walifukuzwa au kulazimishwa kuondoka katika makazi yao ya asili.

 

Hata hivyo, idadi ya Wapalestina waliohama ardhi zao kabla ya kuasisiwa utawala wa Israel inakadiriwa kufikia 350,000. Kwa mujibu wa nyaraka nyinginezo, katika muda wa chini ya miezi 6, tangu Desemba 1947, makundi yenye silaha ya Kizayuni yaliwafukuza Wapalestina wapatao 440,000 kutoka vijiji 220.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa mwaka 2009, idadi ya wakimbizi na vizazi vya Wapalestina waliofukuzwa ambao sasa wametawanyika katika nchi mbalimbali inafikia zaidi ya watu milioni saba.

Sambamba na kuanza kukaliwa kwa mabavu rasmi Palestina baina mwaka 1948 hadi 1950 zaidi ya miji na vijiji 530 vya Wapalestina viliharibiwa. Akthari ya uharibifu huu ulifanywa kwa makusudi ili Wapalestina waliokimbia makazi yao washindwe kurejea katika ardi zao za asili. Katika kipindi cha miaka 75 iliyopita, zaidi ya Wapalestina 100,000 wameuawa kwa risasi za moja kwa moja na watu milioni moja wamekamatwa kwa sababu mbalimbali.

Jinai za sasa za Israel katka Ukanda wa Gaza ni mauaji ya kimbari

 

Mnamo 2021, gazeti la Haaretz lilifichua ukweli kwamba, mamilioni ya nyaraka zinazohusiana na mauaji ya umati zimezuiwa kuchapishwa tangu kuanzishwa kwa serikali ya Israel.

Kwa kuzingatia historia hii chungu na ya kutisha ya matokeo ya Nakba ya Kwanza, inawezekana kusema kuwa, baada ya Israel kuwahamisha wakazi wa Gaza imo mbioni kuwahamishia watu wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hadi Jordan au kuwahamisha Waarabu wa Israel kutoka katika ardhi zilizokaliwa kwa mabavu za mwaka 1948 na bila shaka hili sio jambo lililo mbali na dhana hii.