Watoto wa Gaza; wahanga wakuu wa jinai za utawala wa Kizayuni
Katika kuendeleza jinai zake huko Ukanda wa Gaza jeshi la utawala ghasibu wa Kizayuni Jumamosi tarehe 18 mwezi huu wa Novemba liliishambulia kwa mabomu kwa mara ya pili shule ya Al Fakhoora katika kambi ya wakimbizi ya Jabaliya; ambapo katika jinai hiyo Wapalestina wasiopungua 200 wameuliwa shahidi aghalabu yao wakiwa ni watoto.
Kwa mujibu wa ripoti zote zinazochapishwa kuhusu wahanga na maafa ya binadamu yanayoshuhudiwa huko Gaza, watoto ndio wahanga wakuu wa jinai za utawala huo ghasibu unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu. Takwimu mbalimbali zinathibitisha ukweli huu wa mambo. Hadi sasa watu zaidi ya elfu 12,300 wameuliwa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni; ambapo kati ya mashahidi hao watoto ni zaidi ya elfu 5 yaani watoto wanaunda asilimia 42 ya mashahidi wa Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo ripoti zinaonyesha kuwa watu wengine zaidi ya elfu 30 wamejeruhiwa hadi sasa katika mashambulizi ya utawala haramu wa Israel ambapo asilimia 70 ya majeruhi hao ni watoto na wanawake. Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) limetangaza kuwa, kwa wastani kila dakika 10 mtoto mmoja anapoteza maisha huko Gaza, na wengine 2 pia wanajeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama ya Israel. Mbali na takwimu hizi, makumi ya watoto wachanga pia wanakabiliwa na hatari ya kifo kutokana na kukosekana mafuta ya kuondeshea mitambo katika hospitali za Ukanda wa Gaza.
Nukta muhimu hapa ni kuwa, utawala wa Kizayuni unazishambulia shule kwa makusudi huko Gaza. Utawala huo umezishambulia shule tatu katika ukanda huo katika muda wa chini ya masaa 24 pekee. Jeshi la utawala wa Kizayuni Ijumaa usiku liliishambulia pia shule ya Al Falah kusini mwa Ukanda wa Gaza. Jumamosi iliyopita pia shule ya al Fakhoora inayopatikana kaskazini mwa Gaza ilishambuliwa na jeshi la utawala wa Kizayuni ambapo watu wasiopungua 200 waliuawa shahidi wengi wakiwa ni watoto wadogo. Sambamba na kushambuliwa shule ya Al Fakhoora, shule ya Tal al-Za'atar kaskazini mwa Gaza pia imeshambuliwa kwa mabomu na utawala wa Israel. Matukio yote haya yanathibitisha kuwa utawala wa Kizayuni ambao haujafikia malengo yake kwa kuzishambulia hospitali na vituo vya afya huko Gaza huku kukiwa hakuna taarifa yoyote kuhusu kuwepo mateka wa Israel au njia za chini ya ardhi katika hospitali za Gaza, sasa umezifanya shule za ukanda huo kuwa shabaha ya hujuma na mashambulizi yake.
Suala lingine muhimu ni hili kwamba shambulio hilo la makusudi dhidi ya shule ya Al Fakhoora katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Jabaliya limetekelezwa katika hali ambayo shule hiyo ina mfungamano na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi wa Palestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA). Shirika hilo pia limetangaza kuwa kila siku hutoa taarifa kwa utawala wa Kizayuni kwamba shule na makazi ya wakimbizi yanapaswa kusalia salama pasina kukabiliwa na mashambulizi. Adnan Abu Hasna Msemaji wa shirika la UNRWA huko Ukanda wa Gaza wiki iliyopita alitangaza kuwa shule 50 zenye mfungamano na shirika hilo zimeshambuliwa na jeshi la utawala wa Kizayuni. Pamoja na kuwa watoto wa Kipalestina ni wahanga wakuu wa vita na jinai za Wazayuni, idadi kubwa ya watoto waliosalia hai katika vita hivyo wamepoteza wazazi na ndugu mbalimbali wa familia. Watoto wengi wanaugua maradhi mbalimbali na hakuna uwezekano wa kupatiwa matibabu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kubomolewa, kufungwa na kushindwa kufanya kazi vituo vya afya kutokana na kukosa mafuta na mashambulizi yanayoendelea ya utawala wa Kizayuni.
Kwa utaratibu huo, hata kama hivi sasa pia vita dhidi ya Gaza vitamalizika, lakini idadi ya watoto wa Kipalestina waliouliwa shahidi itaongezeka pakubwa. Hii ni katika hali ambayo jamii ya kimataifa inaendelea kuzikodolea macho jinai za Israel bila kuchukua hatua yoyote; na hakuna uwezekano wa kuchukuliwa hatua Wazayuni na kusitisha mauaji ya watoto yanayofanywa na utawala huo ghasibu kutokana na uungaji mkono wa pande zote wa Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani kwa utawala huo wa Kizayuni.