Al-Wefaq: Bahrain imewasaliti Wapalestina kwa kujiunga na muungano wa US
(last modified Sat, 23 Dec 2023 02:27:55 GMT )
Dec 23, 2023 02:27 UTC
  • Al-Wefaq: Bahrain imewasaliti Wapalestina kwa kujiunga na muungano wa US

Chama kikuu cha upinzani nchini Bahrain cha al-Wefaq kimesema hatua ya utawala wa Aal-Khalifa ya kujiunga na muungano wa baharini wa Marekani katika Bahari Nyekundu ni kusaliti kadhia ya Palestina.

Sheikh Hussain al-Daihi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kitaifa ya Kiislamu ya al-Wefaq amesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa: Taifa la Bahrain haliwezi kunyamazia kimya njama za utawala wa Aal-Khalifa za kulinda maslahi ya utawala wa Israel na jinai zake, na kushiriki katika kuwawekea mzingiro Wapalestina wa Gaza.

Al-Daihi amesema misimamo ya watawala wa Aal-Khalifa ya kuukingia kifua na kuunga mkono utawala haramu wa Kizayuni ni ya kufedhehesha, na kwamba maafisa hao wa Manama wanatakiwa kuliomba radhi taifa sambamba na kujiuzulu.

Siku chache zilizopita Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, alitangaza rasmi kuundwa muungano eti wa kimataifa kwa lengo la kile kinachodaiwa kuwa ni kulinda njia za meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu.

Manowari ya jeshi vamizi la US katika eneo

Austin alisema, nchi za Bahrain, Uingereza, Ufaransa, Italia, Uholanzi, Norway, Ushelisheli na Uhispania ziko katika muungano huo wa baharini. 

Hata hivyo Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza kuwa, vikosi vya Yemen vitaendelea kushambulia meli za kibiashara za Israel madhali utawala huo haramu unaendelea kufanya jinai na kuua raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Kundi kubwa zaidi la upinzani nchini Bahrain la al-Wefaq limesisitiza kuwa, hatua ya watawala wa Aal-Khalifa ya kuupa himaya utawala bandia wa Israel haiwakilishi hata kidogo msimamo wa wananchi walio wengi wa nchi hiyo ya Kiarabu.