Israel yaua watoto wa chekechea katika shambulio la anga Gaza
Kwa akali watoto wawili wa Kipalestina wameuawa shahidi katika shambulizi la anga lililofanywa na ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya shule moja ya chekechea katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Kanali ya Press TV imenukuu ripoti ya shirika la habari la Palestina la WAFA ambalo limeandika kuwa, mbali na watoto wawili wa kike wa shule ya chekechea kuuawa shahidi, wengine kadhaa wamejeruhiwa kwenye hujuma hiyo ya Wazayuni mapema leo alfajiri.
Mkazi wa eneo hilo, Ahmad Bassam al-Jamal ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "Watoto hao walikuwa wamelala, mara ghafla moja mashambulizi ya mabomu yakaanza. Wawili wameuawa huku wengine watatu wakiponea chupuchupu."
Wizara ya Afya ya Palestina imesema idadi ya watu waliouawa katika hujuma za anga za utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Rafah kuanzia usiku wa jana hadi leo alfajiri imeongezeka na kufikia watu 92.
Mwandishi wa al-Jazeera, Hani Mahmoud amesema wakimbizi wa Kipalestina wapatao milioni 1.9 katika mji wa Rafah usiku wa jana walishindwa kulala kabisa kutokana na mashambulizi hayo ya kinyama ya jeshi la Israel dhidi yao.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewauwa shahidi Wapalestina 27,238, aghalabu yao wakiwa wanawake na watoto katika Ukanda wa Gaza, tangu Oktoba 7 mwaka jana, huku wengine zaidi ya 66,000 wakijeruhiwa.
Aidha watoto 25,000 wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza wamebaki mayatima baada ya kupoteza wazazi wao wote wawili au mmoja wao katika vita vya kikatili vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo lililowekewa mzingiro.