Israel imeua zaidi ya watoto 13,000 katika vita vya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i109634-israel_imeua_zaidi_ya_watoto_13_000_katika_vita_vya_gaza
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema zaidi ya watoto Wapalestina 13,000 wameuawa katika vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza. UNICEF imetaja idadi hiyo ya watoto waliouawa kuwa "ya juu" na "ya kutisha."
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Mar 18, 2024 04:11 UTC
  • Israel imeua zaidi ya watoto 13,000 katika vita vya Gaza

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) linasema zaidi ya watoto Wapalestina 13,000 wameuawa katika vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza. UNICEF imetaja idadi hiyo ya watoto waliouawa kuwa "ya juu" na "ya kutisha."

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell alisema Jumapili kwamba pamoja na watoto waliouawa huko Gaza, wengine wengi hawajulikani walipo.

Ameongeza kuwa: "Maelfu zaidi wamejeruhiwa au hatuwezi hata kubaini walipo. Wanaweza kuwa wamekwama kwenye vifusi."

Afisa huyo wa UNICEF amesema:" Hatujaona kiwango hicho cha vifo miongoni mwa watoto katika karibu vita vingine vyovyote ulimwenguni."

Russell pia amesema kwamba watoto wenye utapiamlo katika wodi za uzazi huko Gaza “hawana hata nguvu ya kulia.”

Amelalamika zaidi kuhusu "changamoto kubwa za urasimu" katika kuingiza malori ya misaada katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa, ambapo njaa na utapiamlo mkali vimeenea.

Watoto wa Gaza waliouawa vitani

Utawala dhalimu wa Isareli ulianzisha  vita vya kikatili vinavyoungwa mkono na Marekani dhidi ya Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, kutekeleza operesheni yake ya kihistoria dhidi utawala huo ghasibu ili kulipiza kisasi dhulma zinazozidi kufanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.

Hadi sasa utawala wa katili wa Israel umewaua Wapalestina wasiopungua 31,645 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine 73,676.

Katika uhalifu wa wazi wa kivita, utawala ghasibu wa Isarel sasa unawasababishia njaa watu wa Gaza kimakusudi kwa kuharibu chakula na kuweka vikwazo vikali vya kutoingizwa chakula, madawa na vifaa vingine vya kibinadamu katika eneo hilo.