Jun 17, 2024 03:19 UTC
  • Jeshi la Yemen: Meli mbili zinazozama ni zawadi yetu ya Idi kwa muqawama wa Palestina

Msemaji wa jeshi la Yemen ametangaza kuwa, meli mbili zinazozama ni zawadi ya Eid al-Adh'haa ya jeshi la Yemen kwa muqawama wa Palestina kutokana na kusimama kwao kidete.

Brigedia Jenerali Yahya Saree ameeleza kwamba, kuzama kwa meli za adui ni zawadi ya sikukuu ya Idi ya jeshi la Yemen kwa wananchi na muuqawama wa Palestina ambao umesimama imara kukabiliana na aduii Mzayuni.

Ameongeza kuwa, "Hatma ya meli ambazo zililengwa katika muda wa saa 72 zilizopita kutokana na ushirikiano na bandari zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina zimo katika hali ya kuzama."

Wananchi wa Yemen wametangaza uungaji mkono wao wa wazi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel tangu utawala huo ghasibu ulipoanzisha vita vikali dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba.

Vikosi vya Wanajeshi wa Yemen vimesema kwamba havitasimamisha mashambulizi yao hadi Israel isitishe mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina takriban 37,100 na kuwajeruhi wengine 84,500, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Hivi karibuni Jeshi la Yemen lilishambulia kwa mafanikio meli kubwa ya kivita ya Marekani yenye uwezo wa kusheheni ndege ijulikanayo kama USS Eisenhower na kuilazimu kuondoka karibu na pwani ya Yemen.

Mashambulizi hayo yamelazimisha baadhi ya makampuni makubwa zaidi ya meli za mizigo na mafuta duniani kusimamisha usafiri kupitia mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya baharini katika Bahari ya Sham. Badala yake Meli sasa zinalazimika kuzunguka bara la Afrika badala ya kupitia Mfereji wa Suez.

 

 

Tags