Israel yashambulia tena Nuseirat, Wapalestina 17 wauawa shahidi
(last modified Tue, 18 Jun 2024 07:06:54 GMT )
Jun 18, 2024 07:06 UTC
  • Israel yashambulia tena Nuseirat, Wapalestina 17 wauawa shahidi

Kwa mara nyingine tena, askari wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wamefanya mashambulio ya kikatili kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat na kuua shahidi na kujeruhi makumi ya Wapalestina.

Duru za habari zinaarifu kuwa, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni, usiku wa kuamkia leo zimefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya kambi hiyo iliyoko katikati ya Ukanda wa Gaza, na kuua shahidi Wapalestina wasiopungua 17, mbali na kujeruhi makumi ya wengine.

Aidha wanajeshi makatili wa Israel jana usiku waliwamiminia risasi Wapalestina waliokuwa wanasubiri malori ya misaada ya kibindamu katika mji wa Rafah, na kuua shahidi saba miongoni mwao.

Shirika la habari la WAFA limeripoti kuwa, askari jeshi wa Israel wamevamia vijiji na miji kadhaa huko kaskazini magharibi mwa mji wa Ramallah katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuwatia mbaroni Wapalestina kadhaa.

Jinai za Israel Nuseirat

Ikumbukwe kuwa, Juni 8, jeshi la utawala wa Kizayuni liliendeleza jinai zake za kinyama dhidi ya raia wasio na hatia katika Ukanda wa Gaza, kwa kufanya shambulio la kiwendawazimu dhidi ya kambi ya Nuseirat katikati mwa Gaza ambapo watu 274 waliuawa shahidi, huku idadi ya waliojeruhiwa ikipindukia 700. Iran ni miongoni mwa nchi na asasi za kimataifa zilizolaani vikali jinai ya Nuseirat.

Haya yanajiri huku Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu akitangaza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Ukanda wa Gaza, yameligeuza eneo hilo linalokabiliwa na changamoto nyingi kama umasikini na ukosefu wa huduma muhimu, kuwa Jahanamu ya duniani.

Tags