Kamanda mwingine wa Hizbullah auawa shahidi na droni ya Wazayuni Lebanon
(last modified Tue, 18 Jun 2024 08:06:56 GMT )
Jun 18, 2024 08:06 UTC
  • Kamanda mwingine wa Hizbullah auawa shahidi na droni ya Wazayuni Lebanon

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon inatazamiwa kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya ngome za walowezi wa Kizayuni, baada ya kamanda mwingine mwandamizi wa kundi hilo la muqawama kuuawa shahidi kusini mwa Lebanon.

Katika taarifa, Hizbullah imesema Muhammad Mustafa Ayoub ameuawa shahidi katika shambulio la ndege isiyo na rubani (droni) ya utawala katili wa Israel viungani mwa mji wa Salaa katika wilaya ya Tyre.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, mauaji hayo ya jana Jumatatu yanapelekea idadi ya wapambanaji wa Hizbullah waliouawa shahidi katika mashambulio la Israel kusini mwa Lebanon tokea Oktoba 7, kufikia 343. 

Utawala wa Israel umekuwa ukishambulia mara kwa mara eneo la kusini mwa Lebanon tangu tarehe 7 Oktoba mwaka uliopita, ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Aidha Hizbullah imekuwa ikifanya mashambulizi ya maroketi karibu kila siku dhidi ya maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu (Israel), ili kuonyesha mshikamano wao na Wapalestina wasion na ulinzi wa Gaza.

Haya yanajiri siku chache baada ya Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kufanya mashambulio mapya dhidi ya maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuuni, ikiwa ni kujibu mauaji ya hivi karibuni ya Israel ya kamanda mmoja mkubwa wa harakati hiyo huko kusini mwa Lebanon.

Sami Abdallah 'Abu Taleb' aliuawa shahidi Jumatano iliyopita katika hujuma za anga za Wazayuni zilizolenga jengo la makazi ya watu katika mji wa Jwaya, yapata kilomita 95 kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon.

 

Tags