Walimwengu waendelea kuandamana kuunga mkono Palestina
Maandamano ya kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za Israel huko Gaza yameendelea kufanyika katika mataifa mbalimbali hususan barani Ulaya.
Watetezi wa Palestina katika nchi za Uingereza, Austria, Ujerumani na Italia wamefanya maandamano dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kutoa wito wa kusitishwa vita katika eneo hilo.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu yenye maandishi ya kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za Israel wametoa mwito wa kukomeshwa mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Aidha waandamanaji hao wamezitaka serikali ya Ulaya kuacha kuuuzia silaha utawala haramu wa Israel unaofanya mauaji kila siku dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Waandamanaji hao wameeleza kuchukizwa kwao mno na jinai za Israel dhidi ya wanawake na watoto wadogo wasio na hatia wa Palestina na kuonyesha mshangao wao kwa uzembe wa Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama katika kushughulikia maafa ya Gaza.
Baada ya kupita miezi minane tangu utawala wa Kizayuni uvamie Ukanda wa Gaza bila ya matokeo na mafanikio yoyote, sasa utawala huo unazidi kuzama katika kinamasi cha migogoro ya ndani na nje. Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza kuwa haikubali makubaliano yoyote kati yake na utawala wa Israel unaotekeleza mauaji ya kimbari pasina kusimamisha vita huko Ukanda wa Gaza.