Hamas yakadhibisha madai ya kutumia shule za UNRWA huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i113798-hamas_yakadhibisha_madai_ya_kutumia_shule_za_unrwa_huko_gaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema kuwa madai yaliyotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwepo wapiganaji wake katika shule ya Al-Jaouni katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat ya Ukanda wa Gaza ni ya uongo na ya upotoshaji.
(last modified 2024-07-07T08:57:00+00:00 )
Jul 07, 2024 08:57 UTC
  • Hamas yakadhibisha madai ya kutumia shule za UNRWA huko Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema kuwa madai yaliyotolewa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuwepo wapiganaji wake katika shule ya Al-Jaouni katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat ya Ukanda wa Gaza ni ya uongo na ya upotoshaji.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Palestina, SAFA, Hamas imetoa taarifa ikisisitiza kuwa, madai ya jeshi la Israel kwamba wanachama wa harakati za mapambano walikuwa katika shule ya Al-Jaouni inayosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ambako Wazayuni wamefanya mauaji ya kutisha, ni uongo mtupu.

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa, utawala wa Kizayuni unajaribu kuhadaa maoni ya umma kupitia madai hayo ya uongo na kuficha malengo yake ya mauaji ya watu wa Palestina na uharibifu wa miundombiinui katika Ukanda wa Gaza.

Hamas imesema: Kushambulia na kuharibu makazi 190 ya wakimbizi, shule na vituo vya UNRWA, na mauaji ya mamia ya watu ndani ya kila moja ya makazi hayo, wakiwemo watoto, wanawake na wazee, kunaonyesha sura halisi ya malengo ya baraza la mawaziri la Israel na nia yake ya kubomoa vituo hivyo ili kuendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa, vitendo hivyo dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina na sera ya kuharibu miundombinu na suhula za shirika la Umoja wa Mataifa la UNRWA vinatambuliwa kuwa uhalifu wa kivita na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Hamas pia imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwa na misimamo ya wazi ya kulaani ukatili huo na kuwafungulia mashitaka viongozi wa utawala ghasibu wa Israel. 

Ofisi ya vyombo vya habari vya serikali huko Gaza iliripoti Jana kuwa Wapalestina 16 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 75 walijeruhiwa katika mauaji mapya yaliyofanywa na jeshi la Israel katika shambulio dhidi ya shule ya al-Jaouni katika kambi ya wakimbizi ya al-Nuseirat, ambapo wakimbizi 7,000 wa Kipalestina wamepewa hifadhi.