Lancet: Wapalestina waliouawa Gaza wanapindukia 186,000
Jarida mashuhuri la masuala ya tiba na afya la The Lancet la Uingereza limeripoti kuwa, yumkini idadi halisi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza inazidi watu 186,000.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza, idadi ya Wapalestina waliouwa shahidi hadi hivi sasa tangu jeshi la Israel lianzishe mashambulizi ya kila upande Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023 ni watu 38,000 huku zaidi ya 87,000 wakijeruhiwa.
Hata hivyo, barua iliyoandikwa na wataalamu kwenye jarida la Lancet inasema: Idadi ya waliouawa huenda hata ni kubwa zaidi kutokana na ukubwa wa mgogoro unaoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo la Palestina lililo chini ya mzingiro.
Wamesema, kusambaratishwa miundombinu ya afya, uhaba mkubwa wa chakula, maji na makazi, kushindwa Wapalestina kukimbilia maeneo salama, na kukatiwa ufadhili Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) ni miongoni mwa mambo yanayowafanya waamini kuwa, idadi halisi ya Wapalestina waliouawa Gaza inapindukia 186,000.

Wataalamu hao wanakadiria kuwa, idadi ya maiti za Wapalestina zilizofukiwa na kunasa kwenye vifusi ni zaidi ya 10,000 kwa kuzingatia kuwa, asilimia 35 ya majengo katika Ukanda wa Gaza yamevunjwa na kuharibiwa kikamilifu na mabomu ya Israel, kwa mujibu wa data za Umoja wa Mataifa.
Aidha barua ya waalamu hao iliyochapishwa na jarida la The Lancet la Uingereza imeashiria takwimu za UN zinazosema kuwa, asilimia 90 ya wakazi wa Ukanda wa Gaza wamelazika kuyahama makazi yao kutokana hujuma za kinyama za Israel.