Kuongezeka vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala haramu wa Israel
(last modified Sat, 13 Jul 2024 02:14:18 GMT )
Jul 13, 2024 02:14 UTC
  • Kuongezeka vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala haramu wa Israel

Moja ya hatua za wazi za kuuwekea mashinikizo na kuutenga utawala wa Kizayuni, ambazo zimeshika kasi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kuendelea vita vya umwagaji damu vya utawala huo huko Ghaza, ni kupanuka kwa harakati ya kuisusia Israel katika ngazi za kimataifa.

Kuhusiana na hilo, gazeti la Wall Street Journal la Marekani liliandika katika ripoti yake siku ya Jumatano kwamba, harakati ya kuigomea Israel kufuatia kuendelea vita vyake vya mauaji ya umati katika Ukanda wa Gaza, imekuwa ikipanuka siku baada ya siku katika jamii za Magharibi, hasa baada ya vyuo vikuu kujiunga na harakati hii.

Gazeti la Wall Street Journal likiashiria kwamba harakati hiyo ina uwezo wa kuathiri vyama vya wafanyakazi, taaluma na uchumi wa utawala ghasibu wa Israel, limeandika kuwa kuendelea wimbi la maandamano ya waungaji mkono wa Palestina katika pembe mbalimbali za dunia vikiwemo vyuo vikuu katika nchi za Magharibi na sehemu nyingine za dunia, kumeathiri pakubwa sekta tofauti za utawala wa Kizayuni, ikiwemo ya elimu ya juu. Kwa mujibu wa gazeti hili, Waisraeli sasa wanaona kwamba vyuo vikuu vingi vya Ulaya haviwakaribishi tena wanachuo na wahadhiri wa Israel walio na mafungamano na utawala huo wa kibaguzi.

Uungaji mkono wa kimataifa wa kususiwa Israel

Baada ya kuanza vita vya Gaza kufuatia oparesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023 na jinai zisizo na mfano wake za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu madhulumu wa Gaza, hususan mauaji ya kimbari na utumiaji silaha ya njaa dhidi ya wakazi wa ukanda huo, wananchi wa nchi nyingi wamesimama kupinga jinai za utawala huo. Kwa kuandaa maandamano na mikusanyiko mikubwa, hususan katika nchi za Magharibi, wametaka kukomeshwa uvamizi wa Israel na kufikishwa haraka misaada ya kibinadamu huko Gaza. Maandamano hayo pia yameenea katika ngazi za taasisi za kielimu kama vile vyuo vikuu, ambapo sasa sanjari na kuongezeka mashinikizo ya kutengwa utawala wa Kizayuni, harakati ya kuususia utawala huo imepata msukumo mpya kimataifa.

Wakati huo huo, mashinikizo ya kisheria yameongezeka dhidi ya Israeli kwa njia isiyo ya kawaida, ikiwa ni pamoja na kushtakiwa utawala huo wa kibaguzi katika mahakama za juu zaidi za Umoja wa Mataifa, zikiwemo Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Kabla ya hapo Umoja wa Mataifa ulikuwa umetoa wito wa kuongezwa vikwazo dhidi ya Israel kwa lengo la kuishinikiza ikomeshe vita huko Gaza. Mishael Fakhri, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Chakula, alisema katikati ya Juni mwaka huu kwamba: "Tunachohitaji sasa ni Israel kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kisiasa." Alisisitiza ulazima wa vikwazo vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Israel kutokana na kutofanikiwa mashinikizo ya kisiasa na maombi ya mara kwa mara yasiyojibiwa ya kuitaka Tel Aviv isitishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza.

Hivi sasau utawala wa Kizayuni si tu unashuhudia ongezeko lisilo la kawaida la vikwazo dhidi ya taasisi zake tanzu vikiwemo vyuo vikuu na taasisi za kielimu, bali vikwazo hivyo vimepanuka na kujumuisha ushirikiano wa kijeshi na silaha kati ya makampuni ya Magharibi na Israel. Kuhusu suala hilo, Neta Barak Koren, mhadhiri wa masuala ya sheria katika Chuo Kikuu cha Kiyahudi mjini Quds, ambaye aliunda kundi maalum la kukabiliana na wimbi la vikwazo dhidi ya Israel wakati wa vita vya Gaza, anasema kuwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya taasisi za masomo na elimu ya juu vya Israel vimeongezeka maradufu katika miezi miwili iliyopita, ambapo sasa mashirika na taasisi za kielimu za kigeni zinajiepusha kuamiliana na taasisi za Israel."

Maandamano ya wanaharakati wa kususiwa Israel

Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal, tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza kufuatia operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa tarehe 7 Oktoba, uwanja wa shughuli za harakati inayounga mkono kususiwa utawala huo umekuwa ukipanuka kila siku na kushuhudia mabadiliko makubwa ya msingi. Kutokana na operesheni hii na matokeao ya vita vya Gaza, harakati hii imeweza kufikia baadhi ya malengo yake ya muda mrefu dhidi ya Israel. Harakati ya "Kususia, Kutowekeza na Kuwekewa Vikwazo Israel" (BDS) ni kampeni ya kimataifa ya kuuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni kutokana na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi hizo, ambayo ilianzishwa mwaka 2005 kwa msaada wa Wapalestina 171. Tangu wakati huo, harakati hiyo imeweza kupata wafuasi wengi duniani, ikiwa ni pamoja na katika nchi za Ulaya na Marekani.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni amedai kuhusu harakati hiyo kwamba waanzilishi wake wana nia ya "kuiangamiza Israel." Mkakati wa harakati ya "BDS" ni kufanyika mabadiliko ya taratibu katika kuigomea Israel kwa kuondoa uwekezaji katika nyanja zote za kiuchumi, kisayansi, kitamaduni, michezo na kijeshi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Mkakati wa harakati hii ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za mwaka 1967 umejikita katika kuweka vikwazo na kugomea bidhaa na taasisi za Israel na kuwafahamisha Wapalestina kuhusu umuhimu wa vikwazo hivyo.

Tukiwa tumeingia katika mwezi wa 10 wa vita vya Gaza, vikwazo vimezidishwa dhidi ya Israel katika nyuga mbalimbali, hata katika nchi za Magharibi, zikiwemo za Ulaya, Marekani na Canada, na hivyo kuwadhihirishia wazi watawala wa Kizayuni jinamizi la kuendelea kutengwa kwao katika ngazi za kimataifa.