Hizbullah: Adui anafahamu kwamba, hapaswi kuchukua hatua ya kijinga
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni utachukua hatua ya kijinga utalipa gharama kubwa.
Sheikh Naim Qassem, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema: Netanyahu anapaswa kujua vyema kwamba, iwapo atarefusha vita huko Gaza, utawala huo utaingia katika mchakato wa kuporomoka na kusambaratika zaidi kuliko muqawama na Wapalestina.
Sheikh Naim Qasim, amenukuliwa na duru za habari akisisitiza kwamba, bila shaka adui hawezi kuwa mjinga; kwa sababu anajua vyema kwamba katika hali kama hiyo atalipa gharama kubwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Hezbollah ya Lebanon ameeleza kuwa, kambi ya muqawama nchini Lebanon ilipata nguvu kubwa ya kuzuia mashambulio katika kipindi cha miezi 9 na iliweza kudhibiti vita katika mzuunguko mdogo badala ya vita vikubwa.
Sheikh Naim Qassim ameongeza kuwa: Kambi ya muqawama nchini Lebanon ilisababisha hasara kubwa kwa maadui, ima kwa kuwahamisha takribani watu 100,000 au kwa kusababisha hasara dhidi ya zana za kijeshi na uga wa kiuchumi.
Tangu kuanza kwa vita vya Gaza, mipaka ya Lebanon na ardhi inayokaliwa kwa mabavu yamekuwa uwanja wa mapigano kati ya Hizbullah ya Lebanon na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni. Hizbullah ya Lebanon imesisitiza kuwa, itasimamisha mashambulizi yake dhidi ya utawala wa Kizayuni pale tu hujuma na mashambulio ya Israel dhidi ya Gaza yatakapositishwa.