Jul 17, 2016 07:33 UTC
  • Ukosolewaji mkubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Bahrain

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetoa ripoti yake ya mwaka 2015 hadi 2016 na kutangaza kuwa, Bahrain imeendelea kushuhudia ukandamizaji wa uhuru wa kutoa maoni, mateso na kuendeshwa kesi za kidhulma sambamba na kutolewa hukumu za kidhalimu dhidi ya wapinzani wa kisiasa katika nchi hiyo inayotawaliwa na mfumo wa Kifalme.

Ripoti hiyo ambayo imetathmini na kuchanganua hali ya haki za binadamu nchini Bahrain imetangaza kinagaubaga kwamba, katika miaka ya hivi karibuni Wabaharain 208 wakiwemo watoto wadogo wamepokonywa uraia huku wengine wakilazimishwa kuondoka katika nchi hiyo.

Amnesty International imelaani vikali mateso ya kuratibiwa nchini Bahrain ambayo hufanyiwa watuhumiwa ili kuwalazimisha wakiri mahakamani makosa ambayo hawajayafanya. Ripoti hiyo inakosoa pia jinsi uendeshaji wa kesi dhidi ya wapinzani unavyofanyika pamoja na mazingira ya kesi hizo ambazo huambatana na miamala mibaya na isiyo ya kiutu dhidi ya watuhumiwa ambao hulazimika kukiri makosa ambayo hawajayafanya ili wajisalimishe na mateso.

Sehemu nyingine ya ripoti ya Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International inaeleza kuwa, utawala wa Bahrain umeendelea kukandamiza uhuru wa kutoa maoni, mikusanyiko na uundwaji wa jumuiya na kwa muktadha huo kubana wigo wa harakati hata katika mitandao ya kijamii. Ripoti hiyo inaeleza kwamba, viongozi wa upinzani nchini Bahrain wangali wanasota vizuizini huku wakikabiliwa na anuwai za mateso na unyanyasaji.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, kwa mara nyingine tena maulama wa Bahrain wamefanya mkusanyiko mkubwa na kulalamikia utawala wa kifamilia wa nchi hiyo wa kumpokonya uraia Sheikh Issa Qassim, alimu na mwanazuoni mtajika wa nchi hiyo.

Maulama wa Bahrain wamesisitiza katika mkusanyiko wao huo kwamba, Sheikh Issa Qassim ni mfano wa kuigwa na kiongozi wa kidini nchini Bahrain na kumwandamwa kiongozi huyo maana yake ni kuwaandama Waislamu wote.

Harakati ya Kupigania Haki nchini Bahrain imezitaka nchi za Ghuba ya Uajemi zisishiriki katika kumwaga bure bilashi damu ya wananchi wa nchi hiyo na zisichukue hatua yoyote ile ambayo haina mantiki ndani yake kuhusiana na wananchi wa Bahrain na maulama wa nchi hiyo hususan Sheikh Issa Qassim kwani kinyume na hivyo hawatasalimika na matokeo ya vitendo vyao hivyo.

Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa harakati za amani za upinzani wa wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanapigania uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kutaka kuwepo madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa unatekeleza sera kandamizi za mauaji, kuwahukumu wananchi vifungo vya muda mrefu jela, kuwaweka kizuizini na hata kuwavua uraia wao.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, kuendelea mapambano ya wananchi wa Bahrain kunabainisha na kuweka wazi ukweli kwamba, katika mwaka uliopita wa 2015, mapambano hayo yamechukua mkondo mpana zaidi.

Kwa hakika siasa hizo sio tu kwamba, hazijadhoofisha azma na irada ya wananchi wa Bahrain katika kuendeleza harakati zao dhidi ya watawala wa nchi hiyo, bali ukandamizaji huo umewaimarisha zaidi na kuwafanya wasimame kidete kwa ajili ya kuendelea na malengo yao. Huku utawala wa Aal Khalifa ukiendelea kukosolewa na taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu ulimwenguni, wananchi wa nchi hiyo wameendelea kuandamana ambapo sambamba na kutaka kutekelezwa matakwa yao ya kuweko utawala wa kiaraia, wanatoa wito wa kuachiliwa huru viongozi wa mapinduzi na raia wengine wanaoshikiliwa katika jela na korokoro za utawala huo wakiwemo watoto wadogo.

 

Tags