Lebanon: Hizbullah haijahusika na shambulio la roketi Golan
(last modified Sun, 28 Jul 2024 06:54:31 GMT )
Jul 28, 2024 06:54 UTC
  • Lebanon: Hizbullah haijahusika na shambulio la roketi Golan

Viongozi mbali mbali wa Lebanon wamekanusha vikali madai ya utawala wa Kizayuni wa Israel na vyombo vya habari vya Magharibi eti Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imehusika na shambulio la roketi katika Miinuko ya Golan.

Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri amepuuzilia mbali madai hayo ya Wazayuni na waitifaki wao eti Hizbullah imeshambulia kwa roketi kijiji kimoja kilichoko katika mji wa Majdal Shams, eneo la Golan na kusababisha maafa.

Katika mazungumzo ya simu na Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Berri amesisitiza kuwa, Hizbullah na Lebanon kwa ujumla zinaheshimu sheria na kanuni za vita, na katu hazilengi raia.

Utawala wa Kizayuni wa Israel na vyombo vya habari vya Magharibi vimedai kuwa, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imefanya na shambulio la roketi lililopiga uwanja wa soka katika Miinuko ya Golan, na kusababisha vifo vya watu 11 na kujeruhi wengine zaidi ya 40.

Hata hivyo, Hizbullah imekadhibisha vikali madai hayo na kueleza kuwa, shambulio hilo la jana katika eneo la Majdal Shams yumkini lilisababishwa na mfumo wa kutungulia maroketi wa utawala haramu wa Israel.

Bendera ya Hizbullah ya Lebanon

Afisa Habari wa Hizbullah, Mohammad Afif amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, "Harakati yetu ya Muqawama wa Kiislamu haijahusika kivyovyote na shambulio hilo, na inapinga vikali tuhuma na madai yote bandia dhidi yake." 

Hizbullah inasisitiza kuwa, mashambulio yake ya mwisho yalifanyika juzi dhidi ya Israel, na kwamba ililenga kwa makombora ya kuongozwa mfumo wa kiufundi katika eneo la Ramia na kupiga shabaha moja kwa moja, ambayo imesababisha uharibifu. Imeongeza kuwa, wapiganaji wake walilenga pia mkusanyiko wa wanajeshi wavamizi wa Israel ndani ya eneo la Hadab Yaron.

Wakati huo huo, Najib Mikati, Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon amelaani shambulio hilo dhidi ya eneo la Majdal Shams katika Miinuko ya Golan, huku akiziasa pande hasimu kusitisha uhasama na mashambulizi.