Mwana wa kiume wa Haniya: Wapalestina watapambana mpaka wapate uhuru wao
(last modified Thu, 01 Aug 2024 03:15:25 GMT )
Aug 01, 2024 03:15 UTC
  • Mwana wa kiume wa Haniya: Wapalestina watapambana mpaka wapate uhuru wao

Mwana wa kiume wa Shahidi Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS ambaye aliuawa katika shambulizi lililofanywa katika mji mkuu wa Iran Tehran, ameapa kuwa Wapalestina "watapambana mpaka wapate uhuru wao."

Abdussalam Haniya amesema baba yake "alijitahidi kupigania kwa umoja wa makundi yote ya Palestina," na kwamba kiongozi mkuu huyo wa Hamas alishanusurika majaribio manne ya kumuua.
 
Abdussalam ameongeza kuwa: "Mwenyezi Mungu amemjaalia kifo cha kishahidi ambacho alikuwa akikitamani kila mara". 
 
Mauaji ya Haniya mjini Tehran yametokea chini ya siku moja baada ya utawala wa kigaidi wa Israel kufanya shambulio jengine lililomlenga Kamanda Mkuu wa harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah katika kitongoji cha Beirut, na kuzidisha hatari ya kuzuka makabiliano makubwa zaidi ya kijeshi kati ya Hizbullah na uutawala huo wa Kizayuni.

Mashambulizi ya mfululizo ya kigaidi yaliyofanywa na Israel yameuweka wazi utawala huo haramu kwenye hali ya kuandamwa na visasi vya Hamas, Hizbullah na makundi mengine ya Muqawama katika eneo pamoja na Iran, ambayo imeapa kuwa itatoa jibu kali kwa mauaji ya kiongozi huyo wa Hamas na mshirika wake aliyeuliwa shahidi ndani ya ardhi yake. 

 
Mnamo mwezi Aprili, Iran ilirusha mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani kulenga maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu yaliyopewa jina bandia la Israel kulipiza kisasi cha shambulio la Israel katika majengo yake ya kidiplomasia nchini Syria, ambalo lilisababisha vifo vya washauri kadhaa wa kijeshi wa Iran.
 
Maafisa wakuu wa Hamas nao pia wameapa kuwa jinai ya kigaidi iliyofanywa na Israel ya kumuua shahidi Ismail Haniya haitaachwa bila ya jibu.../