Aug 15, 2024 02:46 UTC
  • Muqawama Iraq: Jibu la Iran dhidi ya Israel litakuwa la nguvu

Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya al-Nujabaa ya Iraq amesema jibu tarajiwa la Iran kwa mauaji ya kigaidi yaliyofanywa mwezi uliopita na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS litakuwa la nguvu, lenye taathira na la kimahesabu.

Sheikh Ali al-Asadi amesema hayo katika mahojiano na Televisheni ya al-Sumaira na kueleza kuwa: "Iran ni nchi ambayo ina sera ya kujibu kupitia shambulio lililokadiriwa na lenye athari."

Asadi amesisitiza kuwa, jibu la Iran litakuwa sawia na uchokozi wa wavamizi kama ulivyotokea katika ardhi yake, na kwa hivyo itajibu kwa kiwango sawa.

Afisa huyo Muqawama wa Iraq amesisitiza kuwa, makundi ya mapambano ya Iraq yatashiriki katika hatua za kulipiza kisasi katika kukabiliana na mauaji yaliyolengwa ya Haniyah na Fuad Shukr mwezi uliopita.

Julai 31, utawala katili wa Israel uliwaua shahidi Ismail Haniyah hapa Tehran na Fuad Shukr, mmoja wa makamanda wakuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon mjini Beirut.

Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya al-Nujabaa ya Iraq pia ameashiria ukatili wa karibuni wa utawala wa Kizayuni ulioua shahidi Wapalestina zaidi ya 100 katika shule ya al-Tabieen inayohifadhi wakimbizi wa Kipalestina mashariki mwa jiji la Gaza na kueleza kuwa, undumakuwili wa Wamagharibi umeipa Israel uthubutu wa kuendelea kufanya jinai na vitendo vya kigaidi.

Sheikh Ali al-Asadi amesisitiza kuwa, makundi yote ya Muqawama katika eneo la Asia Magharibi yatalipiza kisasi cha jinai mtawalia za karibuni za utawala pandikizi wa Israel.

Tags