Mazungumzo ya Doha: Iran yasema Israel, Marekani zinahadaa na haziaminiki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i115316-mazungumzo_ya_doha_iran_yasema_israel_marekani_zinahadaa_na_haziaminiki
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa kauli kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yanayoendelea jijini Doha nchini Qatar, ambapo ameonya kuhusu "udanganyifu na ukosefu wa uaminifu" wa utawala dhalimu wa Israel na muungaji mkono wake muhimu zaidi, Marekani.
(last modified 2024-08-17T01:09:57+00:00 )
Aug 17, 2024 01:09 UTC
  • Mazungumzo ya Doha: Iran yasema Israel, Marekani zinahadaa na haziaminiki

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa kauli kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yanayoendelea jijini Doha nchini Qatar, ambapo ameonya kuhusu "udanganyifu na ukosefu wa uaminifu" wa utawala dhalimu wa Israel na muungaji mkono wake muhimu zaidi, Marekani.

Ali Bagheri Kani alitoa onyo hilo katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Mohammed bin Abdulrahman Al Thani siku ya Ijumaa. Haya yalikuwa mazungumzo yao ya pili ndani ya masaa 24.

Kani aliandika katika chapisho lililochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X Ijumaa jioni kwamba yeye na Waziri Mkuu wa Qatar walibadilishana maoni "kuhusu maendeleo ya siku ya pili ya mazungumzo ya kukomesha mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na  Wazayuni huko Gaza."

Mapema jana, Marekani, Qatar na Misri zilitoa taarifa ya pamoja zikisema zilifanya mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza katika hali nzuri katika jijini Doha. Waliongeza kwamba mazungumzo hayo yalikuwa “mazito, na yenye kujenga.”

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imesema haitakubali masharti mapya kutoka kwa utawala wa Israel kama ilivyoainishwa katika pendekezo jipya.

Kani alisema kuwa Marekani inaipatia Israel silaha jambo ambalo linaifanya kuwa "mshirika wa jinai na sio mpatanishi asiyeegemea upande wowote."

Licha ya mazungumzo ya kusitisha mapigano, utawala wa Israel unaendelea na mashambulizi yake ya anga na mizinga katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa huku vita vya mauaji ya halaiki vikiingia mwezi wake wa kumi na moja.

Tokea Israel ianzishe vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mwezi Oktoba mwaka jana imeua Wapalestina zaidi ya 40,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto