HAMAS: Marekani haina nia ya kweli ya kuhitimisha vita vya Ghaza
Aug 18, 2024 08:44 UTC
Kiongozi Mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, Marekani haina nia ya kweli ya kufanikisha ukomeshaji vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Osama Hamdan, ambaye ni mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon ameeleza kuwa pendekezo jipya la Marekani la kusitisha mapigano halijumuishi kuondoka kikamilifu wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Hamdan amebainisha kuwa wakati mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano bado hayajataja ni wafungwa gani wa Kipalestina wataachiliwa, makubaliano yatakayofikiwa lazima yahakikishe yanaweka vigezo vilivyo wazi ikiwa ni pamoja na vya kuachiliwa huru wafungwa wa Kipalestina.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas ameongeza kuwa, Marekani inajaribu kuupatia utawala ghasibu wa Kizayuni muda wa kutosha wa kuendeleza ukatili zaidi na mauaji ya halaiki.
Vyanzo vya habari vya Misri, ambavyo vimeomba kutotajwa majina, vilinukuliwa jana Jumamosi vikilieza kwamba mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya wawakilishi wa Hamas na Israel ya kutafuta mwafaka wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza yataanza tena Jumatano mjini Cairo.
Kulingana na vyanzo hivyo, wajumbe wa timu za mazungumzo za wapatanishi watatu, yaani Misri, Qatar, na Marekani pamoja na wajumbe wa timu ya utawala wa Kizayuni wa Israel watahudhuria mazungumzo hayo yaliyopangwa kufanyika Jumatano na Alhamisi.
Wawakilishi kutoka Misri, Marekani na Israel kwa sasa wangali wako katika mji mkuu wa Qatar Doha, ambao ulikuwa mwenyeji wa mazungumzo ya hivi majuzi ya kusitisha mapigano yaliyofanyika mapema wiki hii, kujadili "nukta za kiufundi" za makubaliano hayo yakiwa ni maandalizi ya mazungumzo yatakayofanyika mjini Cairo.../