Mchambuzi: Nasrullah amedhoofisha uwezo wa kujihami wa Israel
Mtafiti mmoja wa Kizayuni amekiri uwezo wa Katibu Mkuu wa Hakarati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrallah na kusisitiza kuwa, kiongozi huyo wa Muqawama wa Lebanon amedhoofisha uwezo wa kuzuia mashambulizi wa utawala wa Kizayuni.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimemnukuu Jacques Neriah, mtafiti katika Kituo cha Masuala ya Umma cha Jerusalem (Quds) akisema kuwa, Sayyid Hassan Nasrallah ameonyesha uwezo wa majeshi ya Hizbullah kupitia miji ya makombora ya njia za chini ya ardhi.
Hivi karibuni, Hizbullah kwa mara ya kwanza, ilionyesha picha na video za miji yake ya makombora, ambayo ni ishara ya uwezo wa Muqawama kwa ajili ya kujihama, jambo ambalo limesababisha hofu na wahka miongoni mwa Wazayuni. "Hili ndilo jambo ambalo limesambaratisha nguvu za kuzuia hujuma za Israel," amesema mtafiti huyo wa Kizayuni.
Katika taarifa yake Jumanne asubuhi, Hizbullah ilitangaza kuwa wapiganaji wake wameshambulia vituo vya kijeshi vya Zar'it na Jal Al-Allam kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo ya kaskazini yanayokaliwa kwa mabavu.
Hizbullah imeongeza kuwa, wanamapambano wake pia walilenga vifaa vya uchunguzi vya wavamizi hao katika kambi ya Wazayuni ya Jal al-Allam kwa kutumia ndege isiyo na rubani na kuvisababishia uharibifu mkubwa.
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imekuwa ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara tangu mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana dhidi ya maeneo ya kijeshi ya utawala ghasibu wa Israel ili kulipiza kisasi hujuma za utawala huo ghasibu dhidi ya Gaza na kusini mwa Lebanon.