Jinamizi kwa Wazayuni katika medani ya vita ya kaskazini mwa Palestina
(last modified Sat, 31 Aug 2024 04:16:48 GMT )
Aug 31, 2024 04:16 UTC
  • Jinamizi kwa Wazayuni katika medani ya vita ya kaskazini mwa Palestina

Ingawa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alikusudia kupanua wigo wa vita vya utawala huo kusini mwa Lebanon ili kudhamini maslahi yake binafsi, lakini nguvu ya Hizbullah ya kuzuia mashambulizi na hasa kufanikiwa operesheni yake ya karibuni ya Arbaeen, ambayo imelenga vituo 11 vya kijeshi na kijasusi vya utawala wa Kizayuni, imempelekea kutafakari upya na kuhamishia uchokozi wake katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwa sasa.

Vituo vya matibabu vya Kizayuni vya Al-Jalil na Zif vimekiri kwamba karibu askari elfu 6 wa Kizayuni wamelazwa katika vituo hivyo vya matibabu vya Kizayuni kutokana na majeraha na magonjwa waliyopata wakati wa vita na Hizbullah ya Lebanon. Gazeti la Kizayuni la Yediot Aharonot limekiri kwamba idadi ya askari ambao Kituo cha Matibabu cha Al-Jalil huko Nahariya na Hospitali ya Zif huko Safed zimewapokea kwa ajili ya matibabu imefikia askari 5650.

Huku akitangaza kupokelewa kwa wanajeshi 450 wa Kizayuni waliojeruhiwa katika mapigano ya mpakani na Hizbullah ya Lebanon, Salman Zarqa, mkurugenzi wa Hospitali ya Kizayuni ya Zif, amesema: "Siku za vita bado hazijafika. Idadi ninayoitangaza inahusiana tu na askari ambao wamekuwa wakilengwa moja kwa moja au kujeruhiwa na vipande vinavyotokana na silaha za upande wa adui ambapo kwa maoni yangu, ni idadi kubwa sana."

Ripoti mpya ya Kituo cha Upelelezi wa Ndani katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala huo pia imefichua ukweli unaoashiria hasara kubwa iliyopatikana kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Ripoti hiyo inaeleza kuwa tangu tarehe 8 Oktoba, siku ambayo Hizbullah ilijiunga na muqawama wa Palestina kama "Mhimili wa Kutoa Msaada", zaidi ya makombora 7,500 yamerushwa na harakati hiyo, na takriban roketi 6,500 zimevuka mpaka wa kaskazini wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Kwa kuongezea, zaidi ya ndege 200 zisizo na rubani zimeingia katika maeneo hayo, na wala hali hiyo haionekani kufikia kikomo."

Mashambulio ya Hizbullah dhidi ya Israel

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Ushuru ya utawala wa Israel, tangu kuanza vita huko kaskazini, ripoti za kuharibiwa majengo na makazi 4378 ya walowezi wa Kizayuni katika eneo hilo zimewasilishwa. Mkuu wa moja ya vituo mashuhuri vya utafiti vya Wazayuni pia ametahadharisha kuhusu nguvu za kijeshi za Hizbullah na utayari wa "Kitengo Maalumu cha Rizwan" wa kuingia Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuandika: "Hizbullah ni jeshi kamili lenye mamia ya maelfu ya makombora,  ambalo linaweza kuishambulia Israel wakati wowote." Kuingia  Hizbullah katika vita vya Gaza kumepunguza uzingatiaji wa Israel kwenye uwanja wa vita wa Gaza, na kutuma theluthi moja ya jeshi la utawala huo katika eneo la kaskazini, ambako vitongoji 50 na walowezi Wazayuni elfu 230 wamelazimika kukimbia eneo hili. Kufikia sasa, magari 125 ya kijeshi, vituo 182 vya kamandi, miinuko na ngome 663, vifaa vya kiufundi 450, vitongoji vya makazi 1,050, viwanda vinne vya kijeshi, maghala makuu ya silaha 61, majukwaa 12 ya kuba ya chuma, vituo viwili vya kijasusi, ndege 8 zisizo na rubani na maeneo 825 ya wanajeshi wa Kizayuni yamelengwa na Hizbullah.

Kwa ujumla, kutoweza Netanyahu kufikia malengo yake katika vita vya Gaza kumewafanya maghasibu wa Kizayuni kupinga vitendo vyake vyovyote vipya vyenye gharama na hatari kubwa katika maeneo mengine. Wakati huo huo, uwezo wa Hizbullah katika medani ya vita umethibitishwa mara nyingi kwa Wazayuni. Uwezo huu umebadilisha kanuni za mzozo kwa madhara ya Tel Aviv kwa namna ambayo sasa imeuweka mustakbali na uhai wa utawala huo katika hali ngumu na isiyotabirika.