Hamas: Utawala wa Kizayuni unatekeleza sera za kuwaua kwa makusudi wafungwa wa Kipalestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza katika taarifa yake kwamba adui Mzayuni anatekeleza sera za kuwaua kwa makusudi wafungwa na mateka wa Kipalestina walioko katika magereza ya utawala huo haramu.
Hamas imeeleza katika taarifa yake leo Jumatano kuwa, adui Mzayuni anatekeleza sere za kuwaua kwa makusudi mateka na wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel, na kwamba harakati hiyo kamwe haitalinyamazia kimya suala hilo.
Taarifa ya Hamas imeendelea kueleza: Kuenea magonjwa ya kuambukiza miongoni mwa mateka wa Kipalestina katika magereza ya utawala wa Kizayuni, pamoja na uamuzi wa uongozi wa jela za Israel katika magereza mawili ya "Rimon" na "Nafha" wa kuwazuia wanasheria kukutana na mateka hao ni ushahidi mpya wa hali mbaya inayowasibu mateka na wafungwa wa Kipalestina katika kivuli cha kuendelea ukandamizaji wa taasisi za magereza na kuwanyima raia hao haki zao za msingi za kibinadamu chini ya sheria za kimataifa.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesisitiza kuwa, kukandamizwa wafungwa na mateka wa Kipalestina, ikiwa ni pamoja na kuteswa, kunyimwa fursa ya kuonana na ndugu zao, kuwanyima maji, chakula na usingizi, kutekeleza sera ya makusudi ya kuwanyima huduma muhimu na za dharura za matibabu n.k ni miongoni mwa mnyanyaso na ukandamizaji wanaofanyiwa wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israel, vitendo ambavuo vimepelekea kufa shahidi Wapalestina kadhaa.