Taathira za mauaji ya kigaidi ya Sayyid Hassan Nasrullah kwa mfumo wa dunia
-
Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah
Mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, yanaweza kuchambuliwa katika nyanja mbalimbali, lakini moja ya nyanja hazo ni tathmini ya athari zake katika mfumo wa dunia.
Moja kati ya matokeo na taathira muhimu zaidi ya mauaji ya kinyama na jinai za kutisha za utawala katili wa Israel dhidi ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah katika mfumo wa ulimwengu ni kuonyesha kwamba, mfumo wa dunia unaodai kutetea haki za binadamu na kanuni umeporomoka. Kuanzia miaka ya 1990 na kuendelea mfumo wa dunia ulielekea upande unaotambua kanuni na haki za binadamu kuwa mojawapo ya vyanzo muhimu vya mamlaka. Suala hili lilikuwa muhimu sana kiasi kwamba kwa msingi huo ilianzishwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Moja ya matokeo muhimu ya kuanzishwa mahakama hiyo ni kwamba iliondoa na kufuta hali ya kuwakingia kifua viongozi za nchi wanaotoa amri ya ukiukaji wa haki za binadamu. Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kuwa, mamlakka na utawala vilipata mwelekeo wa maadili. Shambulio lililofanywa dhidi ya Libya mwaka 2011 pia lilitekelezwa kwa msingi huo huo na kwa msingi wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu wa serikali ya Muammar Gaddafi. Vita vya Ukanda wa Gaza na Lebanon na mauaji ya kigaidi ya makamanda na maafisa wa kisiasa, hasa mauaji ya Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, na Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, yamethibitisha kuwa mfumo wa dunia ya leo hautokani na kanuni na haki za binadamu, na haya ni madai ya uongo mtupu.

Matokeo mengine muhimu ya mauaji ya kikatili na jinai za kinyama za utawala bandia wa Israel dhidi ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kwa mfumo wa dunia ni kwamba, kwa mara nyingine tena imethibitisha kuwa, taasisi za kimataifa hazina uwezo wa kusitisha vita na mashambulizi kinyama yanayofanywa na utawala ghasibu za Israel. Mbali na kuwa imepita miezi 11 tangu kuanza mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na jinai zake dhidi ya Lebanon, waziri mkuu mtenda jinai wa Israel Benjamin Netanyahu alitoa amri ya kuuawa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah akiwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York huko Marekani ili aharibu na kutokomeza kabisa hadhi na itibari ndogo ya taasisi hiyo ya kimataifa.
Viongozi mbalimbali wa Umoja wa Mataifa akiwemo Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres, walikuwa wakitangaza mara kwa mara kuwa kinachofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza ni mauaji ya kimbari. Josep Borrell, mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema saa chache tu kabla ya kuuawa Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na utawala dhalimu wa Israel kuwa: "Tunaweka mashinikizo yote ya kidiplomasia kwa ajili ya usitishaji vita na mapigano. Lakini inaonekana hakuna anayeweza kusimamisha (mauaji ya) Benjamin Netanyahu huko Gaza wala Ukingo wa Magharibi." Matamshi haya ya Josep Borrell ni kielelezo cha kuporomoka hadhi na itibari ya Umoja wa Mataifa. Mauaji ya Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah kwa mabomu 80 ambayo kila moja lilikuwa na uzito wa tani moja, yameporomosha zaidi itibari na hadhi ya umoja huo. Huenda taasisi hiyo na asasi nyingine za kimataifa hazitaweza kurejesha heshima na hadhi hiyo iliyotoweka kwa miaka na miongo mingi ijayo.

Matokeo mengine muhimu ya mauaji ya hayati Sayyid Hassan Nasrullah ni kwamba dunia inaelekea kwenye harakati zaidi za kijeshi na silaha. Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unamiliki maghala ya silaha hususan silaha zinazotengenezwa na Marekani, umezidisha jinai dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon. Kinachoupa utawala huo jeuri na ujasiri wa kutenda jinai zisizo na kifani, hasa mauaji ya kimbari, ni maghala hayo ya silaha. Hii leo, ni viongozi wachache sana ambao hawaamini kuwa tunapaswa kuelekea upande wa kuwa na sera za kijeshi, kujizatiti zaidi kwa silaha na kumiliki silaha za kisasa. Matokeo haya muhimu pia yana maana kwamba, mfumo wa kiliberali unaodai kutetea sheria na maadili kimsingi umepoteza utendaji kazi yake.