Madai ya Marekani katika muktadha wa kujaribu kuzuia vita Asia Magharibi
Marekani ambayo ni mdhamini mkubwa zaidi wa silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya mashambulizi makubwa dhidi ya watu wa Lebanon na Gaza, sasa inajitokeza kwa unafiki na kutoa wito wa kupunguzwa mivutano na kurejeshwa amani katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Kwa upande mmoja, Washington inadai kuunga mkono suala la kusitisha vita vya Gaza, na kwa upande mwingine, imetoa silaha na zana za kivita kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya kuishambulia Lebanon na kumuua shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah na makamanda wengine wa harakati hiyo ikidai kwamba uadilifu na haki vimetekelezwa!
Kuhusiana na suala hilo, Rais Joe Biden wa Marekani, akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya pande zote katika Mashariki ya Kati, amesema bila ya kulaani jinai za utawala wa Kizayuni Israel kwamba: Ni lazima tuzuie jambo hili kutokea. Hata hivyo, Rais wa Marekani amekwepa kutoa maelezo zaidi katika uwanja huu. Biden pia ameahidi kumpigia simu Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kuhusu hali ya Mashariki ya Kati na udharura wa kuwepo amani, suala ambalo hakuainisha litafanyika lini.
Matamshi haya yametolewa huku utawala wa Kizayuni ukiendelea kushambulia na kuharibu eneo la Ukanda wa Gaza tangu karibu mwaka mmoja uliopita na kuua na kujeruhi maelfu ya watu, na umefanya mashambulizi yasiyo na kifani dhidi ya Lebanon katika siku za hivi karibuni. Katika uhalifu mwingine mkubwa wa utawala huo, siku ya Ijumaa iliyopita, vikosi vya jeshi la Israel vilishambulia makazi ya raia katika kitongoji cha Hareh Harik mjini Beirut na kuua watu wengi akiwemo Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah.
Vitendo hivi vya kihalifu vya Israel havingewezekana bila msaada mkubwa wa kijeshi na silaha wa Marekani. Hili ni suala ambalo limethibitishwa hata na maafisa na vyombo vya habari vya Marekani. Katika mkondo huo, Seneta wa chama cha Democratic, Mark Kelly, ambaye ni mmoja wa wajumbe waandamizi wa Kamati ya Jeshi ya Seneti ya Marekani amekiri kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umetumia mabomu ya kuongozwa ya Marekani katika jinai ya Ijumaa iliyopita nchini Lebanon. Gazeti la Washington Post pia limechunguza picha zilizochapishwa na jeshi la Israel na kuandika kwamba: Kuna uwezekano mkubwa Israel imetumia mabomu yenye pauni 2000 yaliyotengenezwa na Marekani katika shambulio lake huko Beirut ambalo lilipelekea kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah.
Suala muhimu ni kwamba, Marekani inadai kuwa inajaribu kuzuia vita katika eneo la Magharibi mwa Asia, huku ikiwa ni mfadhili mkuu wa kijeshi na zana za vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unachukua hatua za makusudi za kuanzisha moto wa vita katika eneo la Mashariki ya Kati. Wakati huo huo, maafisa wakuu wa serikali ya Marekani wanaunga mkono waziwazi vitendo vya kigaidi vya Israel, jambo ambalo lina maana ya kumshajiisha mhalifu huyo kuendeleza jinai na uhalifu wake. Kuhusiana na suala hilo, Rais Joe Biden wa Marekani ameitaja hatua ya Israel ya kumuua kigaidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon kuwa ni "utekelezaji wa haki" na kudai: "Hizbullah, chini ya uongozi wa Nasrullah, imehusika na mauaji ya maelfu ya watu, ikiwa ni pamoja na Wamarekani, Waisraeli na Walebanoni kwa kipindi cha miongo minne."
Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris pia, amekariri msimamo wa Joe Biden, na kutaja mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya Sayyid Hassan Nasrallah kuwa ni "utekelezaji wa haki".
Msimamo wa kinafiki na kindumakuwili wa serikali ya Biden kuhusiana na matukio ya hivi majuzi katika eneo la Mashariki ya Kati, hususan uhalifu wa Israel dhidi ya Lebanon, na kukataa Tel Aviv kusitisha vita vya Gaza, vimekabiliwa na ukosoaji mkubwa. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, ameashiria tukio la kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na kusisitiza kuwa, jinai hiyo kwa mara nyingine tena imethibitisha kuwa utawala unaotenda uhalifu wa Israel hauheshimu sheria yoyote ya kimataifa.
Vilevile, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amezungumzia kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni, na kusema, misimamo rasmi ya Iran umetangazwa, na kwa maoni yetu, Marekani ni mshirika katika uhalifu huo na haiwezi kujinasua katika uhalifu huo kwa njia yoyote.