Kambi ya Israel ya Nevatim yapigwa kwa kombora la hypersonic
(last modified Sat, 09 Nov 2024 03:21:24 GMT )
Nov 09, 2024 03:21 UTC
  • Kambi ya Israel ya Nevatim yapigwa kwa kombora la hypersonic

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema vikosi vya nchi hiyo vimefanikiwa kushambulia kambi hasasi ya kijeshi ya Israel ya Nevatim kwa kombora la balestiki la hypersonic.

Saree amebainisha kuwa, operesheni hiyo ilifanywa kwa kutumia kombora la balestiki la hypersonic lililopewa jina la Felestin-2  na kuongeza kuwa, kombora hilo limefanikiwa kulenga shabaha iliyokusudiwa kwa usahihi mkubwa.

Kadhalika Brigedia Jenerali Saree ameongeza kuwa, vikosi vya ulinzi wa anga vya Yemen vimetungua ndege nyingine ya kivita ya Marekani  isiyo na rubani aina ya MQ-9 Reaper katika mkoa wa al Jawf wa kaskazini mwa Yemen, ikiwa ni droni ya 12 ya aina hiyo kuangusha na vikosi vya nchi hiyo.

Hivi karibuni, Harakati ya Ansarullah ya Yemen ilitangaza habari ya kombora lake la hypersonic kupiga kambi ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel mashariki mwa eneo linalokaliwa kwa mabavu la Yafo. 

 Brigedia Jenerali Yahya Saree

 

Wananchi wa Yemen wametangaza uungaji mkono wao wa wazi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, tangu utawala huo pandikizi ulipoanzisha vita vya kutisha dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

Wanajeshi wa Yemen wanasisitiza kuwa, hawatasimamisha mashambulizi yao hadi pale utawala wa Kizayuni utakapositisha hujuma za kinyama huko Gaza, zilizoua Wapalestina zaidi ya 43,469 hadi sasa.